MOSHI.
Katika kuadhimisha Wiki ya Mazingira, Bodi ya Maji Bonde la Pangani imezindua kampeni maalum yenye lengo la kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki katika vyanzo vya maji.
Kampeni hiyo imepewa jina “Kila Unapoona Plastiki – Okota”, na inalenga kuhamasisha jamii kutunza mazingira kwa vitendo.
Akizungumza Juni 3,2025 katika zoezi la upandaji miti zaidi ya mia tano kwenye chanzo cha Mto Rau, katika eneo la chemchem ya Sabasaba, Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi, Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Mhandisi Segele Segule, amesema plastiki zimekuwa tatizo kubwa kwenye mito na chemchem, na zinahatarisha maisha ya binadamu na viumbe wa majini.
Alisema uchafuzi wa mazingira unaotokana na chupa za plastiki ni tatizo linalokua kwa kasi, hivyo tunapaswa kuelimisha jamii namna ya kuhifadhi na kutumia plastiki kwa uangalifu, badala ya kuzitupa ovyo.
Aidha alisisitiza kuwa matumizi ya plastiki siyo mabaya, lakini matumizi holela na utupaji usio rasmi ndio unaosababisha madhara, ameishauri Manispaa ya Moshi kuanzisha vituo rasmi vya kukusanyia plastiki na kutoa elimu katika maeneo ya umma, kama vile stendi za mabasi, vijiwe vya bodaboda, bajaji na mashule.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Mhandisi Araf Majid, alisema katika wiki hii ya mazingira, bodi hiyo itafanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuweka alama za mipaka kwenye vyanzo vya maji, kufanya usafi katika mito mikuu kama Mto Rau, Njoro na Kijenge, kwa kushirikiana na halmashauri husika.
Alisema pia watatoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za plastiki, kwa kuzingatia Kaulimbiu ya Taifa inayosema: Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo – Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki."
Katika zoezi hilo la upandaji miti, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Mto Rau, Habibu Hashim Lema, alisema kuweka miti katika vyanzo vya maji ni njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira na kuongeza uoto wa asili.
Nao wakazi wa mtaa wa Sabasaba, waliounga mkono kampeni hiyo, wamesema plastiki zisipotupwa vizuri huishia kwenye mito, na baadaye kuathiri samaki na afya ya binadamu.
Mmoja wa wananchi hao, Denis Mlay, alisema upandaji miti ni jambo muhimu sana kwa mazingira yetu, kwani wanaitumia miti kwa kila hali ya maisha, hivyo wanapaswa kuilinda ambapo pia amesema plastiki zinaweza kuwa biashara nzuri badala ya kuzitupa hovyo.
Kwa ujumla, Bodi ya Maji Bonde la Pangani imetoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo, hasa plastiki, ambazo zimesababisha madhara makubwa kwenye vyanzo vya maji.















