SERIKALI YAJIPANGA KUGHARAMIA BAJETI KWA FEDHA ZA NDANI

BUNGENI-DODOMA

Serikali imesema inaendelea na jitihada mbalimbali za kuongeza mapato ya ndani, ili kugharamia bajeti ya nchi kwa kutegemea zaidi vyanzo vya ndani, badala ya kutegemea misaada kutoka nje.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi.

Katika swali lake, Mbunge Ndakidemi alitaka kujua ni kwa namna gani serikali imejiandaa kukabiliana na mabadiliko ya sera za baadhi ya nchi tajiri ambazo zimeanza kupunguza misaada ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea, zikiwemo Tanzania.

Dkt. Mwigulu alijibu kwa kusema "Serikali imeweka mkazo katika kuongeza mapato ya ndani ili kugharamia miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kibajeti kwa kutumia rasilimali zetu wenyewe, jambo ambalo litasaidia kupunguza utegemezi kutoka kwa washirika wa maendeleo."

Aidha, alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kugharamia miradi ya maendeleo, kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, maarufu kama PPP – ili kupunguza mzigo wa mikopo.

Kuhusu maswali ya nyongeza kutoka kwa Profesa Ndakidemi, ikiwemo kuhusu uamuzi wa Marekani kusitisha misaada kwa baadhi ya nchi, Waziri Nchemba alieleza kuwa Tanzania haikuwa inapokea misaada ya moja kwa moja ya miradi ya maendeleo kutoka serikali ya Marekani.

Alifafanua kuwa misaada mingi kutoka Marekani imekuwa ikipitia taasisi za kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi nchini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.