WAATHIRIKA WA MAFURIKO MBOKOMU WAPOKEA MSAADA KUTOKA SERIKALINI, WAISHUKURU SERIKALI

MBOKOMU-MOSHI

Katika hatua ya kuonyesha mshikamano na kuwajali wananchi wake, serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi imetoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko katika Kata ya Mbokomu, yaliyotokea mwezi Mei mwaka huu.

Mafuriko hayo, yaliyoikumba sehemu ya mtaa wa Mbughuni katika Kijiji cha Korini Kusini, yalisababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine watatu waliolazwa kwa wiki kadhaa katika Hospitali ya St. Joseph, ambapo nyumba kadhaa ziliharibiwa, ikiwemo ya familia ya Zacharia Shija, ambayo ilisombwa kabisa na mafuriko hayo makubwa.

Katika tukio la kugawa misaada kwa waathirika, Diwani wa Kata ya Mbokomu, Raphael Materu, alikabidhi misaada hiyo Juni 3,2025 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, alieleza kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele tangu siku ya tukio, kuanzia kuokoa maisha, kugharamia matibabu hadi kusaidia kurejesha matumaini ya maisha mapya kwa waathirika.

“Serikali kupitia kamati ya maafa ya wilaya imetusaidia kwa kiasi kikubwa, gharama za matibabu zilizofikia zaidi ya milioni 2.7 zilibebwa kikamilifu pia, tunashukuru kwa misaada ya vyakula, malazi, na mahitaji ya shule kwa watoto,” alisema Materu.

Misaada iliyotolewa ilihusisha mablanketi, magodoro, mashuka, gunia la mahindi, jiko la gesi, vyombo vya kupikia na usafi, nguo, pamoja na madaftari na kalamu kwa watoto walioko shule ambapo pia, waathirika walipatiwa nyumba ya muda kwa ajili ya kuishi kwa kipindi cha miezi mitatu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Mratibu wa maafa na majanga Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Zacharia Dionis, alieleza kuwa tukio hilo limeongeza uelewa wa athari za mabadiliko ya tabianchi, na kutoa wito kwa wananchi wa maeneo hatarishi kuhama mapema na kujenga kwenye maeneo salama zaidi.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka miwili 2024 hadi mwaka 2025 watu wanane wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo ya juu ya wilaya ya Moshi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Korini Kusini, Alen Ngowi, aliwataka wakazi wa maeneo ya mabonde kuzingatia ushauri wa serikali na wataalamu wa mazingira, akisisitiza kuwa maisha ni muhimu kuliko mali.

Naye Katibu wa UVCCM Kata ya Mbokomu, Philibet Macha, alitoa pongezi kwa serikali na viongozi wa eneo hilo kwa kujitokeza mara moja kusaidia. “Hatua hizi zimeleta faraja kubwa kwa wananchi na kuonyesha kuwa serikali iko pamoja na watu wake wakati wa shida,” alisema.

Waathirika waliopokea misaada hiyo walionyesha hisia za shukrani, wakieleza kuwa msaada huo umewasaidia kurudia hali ya kawaida taratibu.

“Tulikuwa hatujui pa kuanzia baada ya kupoteza kila kitu, lakini msaada huu umetuwezesha kuanza tena,” alisema Zacharia Shija, mmoja wa waathirika.

"Mafuriko haya yanabaki kuwa kumbukumbu ya uchungu lakini pia ya mshikamano wa kijamii na uongozi unaojali, Serikali imesisitiza kuendelea kuchukua hatua za kuzuia maafa kama haya kwa kuhimiza ujenzi wa miundombinu salama na uhamasishaji wa jamii kuhusu hatari za mazingira," alisema Antusa Kessy.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.