CHUO CHA VIWANDA VYA MISITU MOSHI- FITI KUANZISHA KOZI TATU MPYA ZA VETA KUKABILIANA NA WIMBI LA UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA

MOSHI.

Katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini, Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kimepata idhini ya kuanzisha mafunzo mapya ya ufundi stadi chini ya VETA katika kozi tatu muhimu zinazohusiana na sekta ya misitu.

Akizungumza Juni 4,2025 na Waandishi wa habari Makamu Mkuu wa Chuo hicho upande wa Utawala na Fedha, Sadikiel Mtui, alisema kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026, chuo kitaanza kutoa kozi za Uhudumu wa Misitu, Uselemala, na Uchakataji wa Mazao ya Misitu, zote zikitolewa kuanzia ngazi ya kwanza hadi ngazi ya tatu.

"Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wanaohitaji mafunzo ya ufundi stadi, tumeona ni muhimu kuanzisha kozi hizi ambazo zitawawezesha wahitimu kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu, ikiwa ni pamoja na kuzalisha nishati safi ya kupikia kutokana na mabaki ya mazao ya misitu," alisema Mtui.

Alibainisha kuwa kozi hizo zitaandaa vijana kuwa wataalamu wa uhifadhi na usimamizi wa misitu, wakiwemo wale wanaohusika na ukusanyaji wa mbegu, uanzishaji wa vitalu vya miche, upandaji miti na matumizi bora ya mazao yake.

Alisema wahitimu wa kozi ya uselemala wataweza kutengeneza bidhaa mbalimbali kama samani, na wale wa uchakataji wa mazao ya misitu watahitimu wakiwa na ujuzi kamili wa kusindika malighafi za misitu kwa njia ya kitaalamu na yenye tija.

Aidha Makamu Mkuu wa Chuo hicho aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kujiunga na kozi hizo mpya, ambazo zinafungua milango ya ajira, ujasiriamali na mchango chanya katika uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wao, wanafunzi wa chuo hicho walieleza jinsi ambavyo elimu wanayoipata imekuwa na manufaa makubwa kwao na kwa jamii.

Mwanafunzi Pendael Ami alisema, “Chuo hiki kimebeba thamani ya mnyororo mzima wa mazao ya misitu. tunatarajia kujiajiri kwa kutumia stadi tunazopata hapa."

Mwanafunzi mwingine wa FITI Clinton Peter, alisema, “Chuo kinatusaidia kukuza ujuzi wa misitu na utunzaji wa mazingira, tunafundishwa namna ya kuzalisha miche ya miti, jambo ambalo linatufungulia fursa za kujipatia kipato baada ya kuhitimu.”




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.