MOSHI.
Kiwanda cha sukari cha TPC kimeungana na wadau mbalimbali wa mazingira kuchangia juhudi za kuokoa Mlima Kilimanjaro, kwa kutoa mchango wa Sh milioni 20, sawa na miti zaidi ya 10,000 katika kampeni ya upandaji miti inayolenga kulinda mazingira ya mlima huo maarufu duniani.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa TPC, wakati wa tukio la upandaji miti lililofanyika katika lango kuu la Marangu, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Alen Maro alisema kuwa kiwanda hicho kimeamua kushiriki kikamilifu katika juhudi za kitaifa na kimataifa za kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro, kwa kuwa wao ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa rasilimali zinazotoka mlimani humo.
“Kwa mara ya kwanza tumeamua kushiriki katika tukio hili muhimu, Sisi TPC ni wadau wa mazingira lakini pia tunanufaika moja kwa moja na maji yanayotoka katika mito inayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro, uhai wa mlima huu ni uhai wa shamba letu la miwa, na hatimaye usalama wa chakula na sukari,” alisema Maro.
Alisema kuwa mfumo wa umwagiliaji unaotegemewa na shamba hilo hutumia maji ya mito inayotiririka mwaka mzima kutoka Mlima Kilimanjaro, hata katika vipindi vya ukame, hivyo ni muhimu kuhifadhi mazingira ya mlima huo ili kulinda vyanzo vya maji na maisha ya wakazi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Maro alieleza kuwa TPC imekuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 10,000 kila mwaka, pamoja na kugawa miche kwa vijiji vinavyozunguka kiwanda hicho na taasisi mbalimbali.
“Tumekuwa tukifanya haya kwa miaka mingi, na juhudi hizo zimeisaidia TPC kupata Tuzo ya Rais ya Utunzaji wa Mazingira, pamoja na tuzo nyingine za mkoa na kanda, hii ni chachu ya kuendelea kufanya zaidi,” alibainisha.
Aidha, Maro alisisitiza umuhimu wa kuulinda Mlima Kilimanjaro kutokana na faida nyingi unazotoa kwa taifa, ikiwemo utalii, ajira, maendeleo ya biashara na huduma kwa jamii.
Naye Mkurugenzi Taasisi isiyo ya kiserikali ya Nessa Foundation inayojihusisha na mazingira, kupitia Kampeni ya “Save Mount Kilimanjaro Campaign Deborah Nyasinda alisema “Zaidi ya watu 65,000 walitembelea Mlima Kilimanjaro ndani ya kipindi cha miaka miwili".
Alisema wageni hao walilala katika hoteli zetu, walikula chakula chetu, na kupitia wao watu wa hapa walijenga nyumba, waligharamia elimu ya watoto na huduma nyingine muhimu,” alisema.
Aliongeza kuwa fedha zitokanazo na utalii wa mlima huo huingizwa kwenye uchumi wa taifa na kusaidia katika ujenzi wa barabara, hospitali, shule na kununua dawa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuunga mkono juhudi za kuhifadhi mlima huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya upandaji miti kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, alisisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.
“Serikali inasisitiza kila mmoja kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti, na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, tishio la kuyeyuka kwa theluji ya Mlima Kilimanjaro ni la kweli, na linahusiana moja kwa moja na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mwangwala.
Mwangwala aliongeza kuwa hatua za kukabiliana na hali hiyo ni pamoja na uelimishaji wa jamii, uboreshaji wa sera za mazingira, na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala rafiki kwa mazingira.
TPC YACHANGIA MILIONI 20 KUOKOA MAZINGIRA YA MLIMA KILIMANJARO
0
June 01, 2025
