KNCU KUKUSANYA KILO 150,000 ZA KAHAWA MSIMU WA 2025/26

MOSHI.

Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU 1984) Limited kimetangaza mpango wa kukusanya zaidi ya kilo 150,000 za kahawa kwa msimu wa 2025/26, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka kilo 36,305 zilizokusanywa msimu uliopita wa 2024/25.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 40 wa chama hicho uliofanyika mjini Moshi, Mwenyekiti wa KNCU, Julius Mollel, alisema mafanikio hayo yanatarajiwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji kwa wanachama wake.

"Iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri, tunatarajia kukusanya kilo 150,000 msimu ujao kutoka kwa vyama wanachama 14, tofauti na msimu uliopita ambapo tulikusanya kilo 36,305," alisema Mollel.

Kwa mujibu wa Mollel, KNCU inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji, ikiwemo, usambazaji wa miche 31,000 ya kahawa kwa wakulima, uanzishaji wa vitalu vitatu vya miche vitakavyokuwa na uwezo wa kuzalisha miche 300,000 kwa mwaka, ambayo itasambazwa kwa wakulima kuongeza tija mashambani.


Aidha, Mollel alisema chama hicho kinaongeza juhudi za kutafuta masoko ya kimataifa kwa kuuza kahawa moja kwa moja katika nchi za China, Finland, Ubelgiji na Japan kama njia ya kuongeza mapato kwa wakulima wake.


Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava aliipongeza KNCU kwa juhudi zake katika kuendeleza zao la kahawa.

"Miongoni mwa hatua nzuri ni pamoja na kuongeza bei ya kahawa kutoka Sh 6,000 kwa kilo msimu wa 2023/24 hadi kufikia Sh 9,640 msimu wa 2024/25," alisema.


Aidha, Mnzava alisema kuwa kuanzia msimu wa 2025/26, KNCU imeondoa malipo ya ushuru kwa kahawa ghafi ya wakulima, hatua inayolenga kurejesha fedha zaidi kwa mkulima ili kuongeza motisha ya kuzalisha.

"Serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na KNCU na wadau wengine kuhakikisha uzalishaji wa kahawa unaongezeka mwaka hadi mwaka," alisema Mnzava.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa KNCU (1984) Ltd, Dkt. Honest Kessy, alisema chama hicho kimeanza kuboresha mikataba inayohusiana na mashamba yanayomilikiwa na chama ili kuongeza ufanisi wa kiuchumi kupitia rasilimali zake.

"Tunaendelea pia kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa wakulima kuhusu uzalishaji wa kahawa bora, kwa kuwa ubora wa kahawa huamua bei sokoni na pia kuchangia uchumi wa Taifa," alisema Dk Kessy.


Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ushirika, wadau wa kahawa, maofisa wa serikali na wanachama wa KNCU kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro.


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava


Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU 1984) Limited Julius Mollel

      Mtendaji Mkuu wa KNCU (1984) Ltd, Dkt. Honest Kessy


Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Kilimanjaro Jacqueline Senzighe







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.