WAFUGAJI HAI WATAKIWA KUFUGA KISASA

HAI-KILIMANJARO.

Wafugaji wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro wametakiwa kubadili mtazamo wa ufugaji wa mazoea na kuanza kufuata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa afya ya mifugo ili kuongeza tija na kudhibiti magonjwa kwa ufanisi zaidi.

Wito huo umetolewa na mdau wa maendeleo wilayani humo, Fuya Kimbita, wakati akifunga mafunzo na kukabidhi vyeti kwa wafugaji na maafisa mifugo, mafunzo yaliyokuwa yameandaliwa na Shirika lisilo kuwa la kiserikali la Community Empowerment Toward Sustainable Development (CETOSUDE) kwa ufadhili wa GAD Foundation na Wild Ganzen kutoka Uholanzi.


Kimbita alisema hakuna tija kwa wafugaji wanaoendelea kutumia mbinu za jadi bila kuzingatia tiba na ushauri wa kitaalamu, hivyo ni muhimu kuhamasisha matumizi ya mbinu za kisasa.

"Niwapongeze wafugaji kwa utayari wenu wa kupokea mafunzo haya, huu ni mwendelezo wa elimu mliyopata awali. Niwashukuru pia CETOSUDE kwa kuja na wazo hili la kuwajengea uwezo wafugaji," alisema Kimbita.

Aidha, alihimiza wafugaji kuachana na ufugaji wa kienyeji na kuanza kufuga kwa njia za kitaalamu ili wapate maziwa mengi, nyama bora, na mifugo yenye afya.


"Wafugaji hawawezi kufikia tija ya kweli ikiwa wataendelea kutumia tiba zisizo na uhakika. Ninyi kama wahitimu wa mafunzo haya, mnapaswa kwenda kuwaelimisha wengine kwa kutumia maarifa mliyoyapata hapa," aliongeza.


Akizungumzunza Mkurugenzi Mtendaji wa CETOSUDE, Joseph Massawe, alisema mradi huo unatekelezwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania katika kata tatu za  Machame Uroko, Machame Kaskazini na Machame Kusini, zilizoko wilaya ya Hai mkoani hapa.

Alisema tayari wameanza na wafugaji 60 na maafisa mifugo 20 huku malengo ni kuwafikia wafugaji zaidi ya 300.

“Mchakato wa maandalizi ulianza Septemba 2023 baada ya wataalamu kutoka Uholanzi kushirikiana na mtaalamu kutoka Kenya na timu ya CETOSUDE kutembelea maeneo mbalimbali kufanya tathmini ya changamoto na fursa zilizopo kwa wafugaji wa maeneo haya,” alisema Massawe.

Tathmini hiyo ilifanikisha maandalizi ya pendekezo la mradi ambalo lilizingatia mahitaji halisi ya jamii ya wafugaji. Mradi ulizinduliwa rasmi Novemba 2024, ukilenga kuwawezesha vijana, wanawake na makundi maalumu yaliyo katika mazingira magumu.

Massawe alisema, kwa kushirikiana na wafadhili wao, CETOSUDE imenunua mashine tatu za kuchakata majani kwa ajili ya lishe bora ya mifugo, ambapo kila kata imenufaika kwa mashine moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na Uzalishaji wa Mazao na Kilimo Global Agriculture Development Foundation (GAD), Michael Maunda, alisema mradi huo umetekelezwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya  kwa miaka mitatu na wakulima wamepata mafanikio makubwa.


"Leo hii kuna wakulima wanakamua kwa siku moja maziwa lita 33 kwa ng'ombe mmoja,  lakini hapo awali walikuwa wakikamua kwa siku moja lita tatu hadi tano,"alisema.

 
Baadhi ya wafugaji walionufaika na mashine hizo, Raymond Nyaki na Rose Tesha waliishukuru CETOSUDE kwa kuwapatia elimu itakayowawezesha kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya sekta ya ufugaji.


“Mafunzo haya yametupa suluhisho kwa changamoto kama ukosefu wa malisho bora. Tumefundishwa jinsi ya kutengeneza chakula maalum cha ng'ombe (silage) kwa kutumia mabua ya mahindi, maharagwe na mpunga,” Walisema.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.