MOSHI-KILIMANJARO.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2025.
Chaulo alitoa wito huo jana wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa kushirikiana na Wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa PCCB House, ikiwa na lengo la kujadili mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi.
"Niwashukuru nyote kwa kuitikia wito huu na kufika kushiriki pamoja nasi kwenye warsha hii, tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuhakikisha wananchi wa Kilimanjaro wanapata taarifa sahihi, hasa kuhusu mapambano dhidi ya rushwa," alisema.
Alibainisha kuwa warsha hiyo inalenga kuwajengea waandishi wa habari uelewa wa kina na uwezo wa kuchukua hatua thabiti katika kuzuia na kupambana na rushwa katika mchakato mzima wa uchaguzi, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikumbwa na changamoto hiyo.
“Rushwa katika uchaguzi ni tishio kwa demokrasia. Inaharibu uwazi wa mchakato wa uchaguzi, kupotosha maamuzi ya wapiga kura, na mara nyingine huzalisha viongozi wasiowajibika, hali hiyo hupunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya uchaguzi na hatimaye kuhatarisha amani ya taifa,” alieleza.
Chaulo alisema kuwa wanahabari wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha kuwa demokrasia na uwajibikaji vinaimarika kupitia taarifa zinazowafikia wananchi, ambapo pia aliwasihi wanahabari hao kuzingatia maadili ya taaluma yao, kuwa waadilifu, na kuepuka kuwa sehemu ya mfumo wa rushwa.
“Wanahabari mnapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si chanzo cha tatizo la rushwa, hakikisheni mnatenda haki, mnapaza sauti dhidi ya wahusika wa rushwa, na msiegemee upande wowote, muwe na dhamira ya kweli ya kusaidia mkoa wa Kilimanjaro kuondokana na rushwa,” alisema.
Aidha, alisema kuwa TAKUKURU iko tayari kushirikiana na wanahabari katika kutoa elimu ya kupambana na rushwa kwa jamii, na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki siasa safi kwa amani na uadilifu.
“Wanahabari mna jukumu kubwa la kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa, hasa katika uchaguzi, mwaka huu tunao uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, tumeona ni vyema tukutane mapema ili tujadili kwa kina namna bora ya kushirikiana katika mapambano haya,” aliongeza.
Chaulo alisisitiza kuwa iwapo wanahabari watachukua nafasi yao ipasavyo, jamii itakuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa misingi ya haki, usawa na maendeleo ya taifa.