TIMU YA WARATIBU WA MAAFA YAWASILI MOSHI KUFUATIA VIFO VYA WATU WATATU KWA MAPOROMOKO YA UDONGO

MOSHI.

Timu ya Waratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, imeweka kambi maalum wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kufuatia maporomoko ya udongo yaliyojitokeza katika Kata ya Mbokomu na kusababisha vifo vya watu watatu, wakiwemo wawili wa familia moja.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 6, 2025, baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya milimani na kusababisha maporomoko yaliyobomoa nyumba na kusomba baadhi ya wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza Mei7,2025 katika maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) yaliyofanyika mjini Moshi, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema mvua hizo zimeleta madhara makubwa, hasa katika maeneo ya tambarare yanayopokea maji kutoka maeneo ya juu ya mlima.

Aidha, amebainisha kuwa watu wengine wanne walijeruhiwa katika tukio hilo ambapo kwa sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Joseph iliyopo mjini Moshi.

Mnzava amesema mvua hizo zilianza kunyesha tangu mapema mwezi Aprili, lakini athari kubwa zaidi zimeanza kushuhudiwa Mei,  ambapo maporomoko ya udongo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na makazi ya watu.

Aidha alisema Serikali ya wilaya imetoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi maeneo ya milimani au mabondeni kuchukua tahadhari kubwa, ikiwa ni pamoja na kuhamia maeneo salama kwa muda hadi hali itakapotengemaa.

Akizungumza Diwani wa Kata ya Mbokomu, halmashauri ya wilaya ya Moshi Raphael Materu, alisema tukio hilo limeacha majonzi makubwa kwa wakazi wa kata yake, hasa kutokana na namna lilivyotokea ghafla usiku wakati wengi wakiwa katika usingizi. 

Amesema hilo ni tukio la pili kutokea ndani ya kata yake ambapo mwaka jana mwezi Aprili 2024, yalitokea mafuriko kama hayo na kupoteza wananchi kwa kuangukiwa na ngema usiku wakiwa wamelala na hili ni tukio la pili kutokea ambalo limetokea Mei 5, mwaka huu pia limeweza kupoteza maisha ya wananchi  watatu.

Aidha alisema tayari wameanza jitihada za pamoja za kuwasaidia waathirika kwa kuwapatia mahitaji ya msingi na kuwashauri kuhusu hatua za usalama, lakini pia tunazidi kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi wetu walioko kwenye maeneo ya hatari.

Aliongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha kuwa serikali inapeleka misaada ya haraka na kuchukua hatua za muda mrefu kama kuhamasisha ujenzi salama, kuzuia ukataji wa miti hovyo milimani, pamoja na kuboresha mifereji ya maji ili kupunguza hatari ya maafa ya baadaye.
















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.