WANAWAKE 300 WAJASIRIAMALI WA KATA YA NJIAPANDA WAPATIWA MIAVULI YA KUJIKINGA NA MVUA NA JUA

NJIAPANDA-HIMO.

Wanawake 300 wajasiriamali wa Kata ya Njiapanda, Mji Mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa miavuli maalum kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt. Charles Stephen Kimei, kama sehemu ya juhudi za kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku kwa ufanisi zaidi.

Miavuli hiyo itawawezesha kuepuka madhara ya mvua na jua, na hivyo kurahisisha mazingira ya kufanya biashara zao.

Hatua hii ni muendelezo wa juhudi za Mbunge Dkt. Kimei katika kuboresha ustawi wa wananchi wake, hasa wajasiriamali wanawake, na inalenga kunufaisha zaidi ya wajasiriamali 2,000 katika Jimbo la Vunjo.

Kwa msaada huu, wajasiriamali wanawake wanatarajiwa kufanya biashara zao kwa amani, huku wakizingatia ufanisi na ustawi wa shughuli zao.

Wakizungumza baadhi ya wajasiriamali hao waliopatiwa misaada hiyo walimshukuru Mbunge Kimei kwa msaada wake mkubwa, na kumchangia kiasi cha shilingi 260,000 kama mchango wa hiari ili kumsaidia kuchukua fomu ya kuomba uteuzi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), atakapojitokeza tena kugombea ubunge katika uchaguzi ujao.

Kitendo hiki kinadhihirisha imani kubwa waliyonayo kwa Mbunge wao kutokana na kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Vunjo.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.