MOSHI.
Serikali ya Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kiliamanjro, imesema moja ya changamoto kubwa inayoikumba wilaya hiyo kwa sasa ni vitendo vya ushoga, usagaji, ulawiti na ubakaji, licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kupambana na hali hiyo kupitia sheria na kampeni za elimu kwa umma.
Akizungumza Mei 7, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) yaliyofanyika katika Kanisa la Anglikana Holy Trinity mjini Moshi, Mkuu wa Wilaya ya Mosho Godfrey Mnzava amesema vitendo hivyo vinaendelea kuongezeka na kuwa changamoto kwa jamii ya mkoa wa Kilimanjaro.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kusikitishwa na namna baadhi ya watu hususan vijana wanavyojihusisha na vitendo hivyo bila aibu, hali ambayo amesema haikuwahi kushuhudiwa kwa kiwango hicho katika mkoa huo.
Alisema kuwa mataifa makubwa yaliyoendelea yamekuwa mstali wa mbele kuhamasisha ushoga na usagaji kwa mataifa ya Africa kwa ajili ya manufaa yao na sio kwa manufaa ya Africa na kuwaomba Maaskofu, na Wachungaji kuendelea kukemea vitendo hivyo kwa nguvu zote vitendo vya ushoga na usagaji, vinavyoharibu watoto kwa sasa.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini na wadau mbalimbali kuelimisha jamii ili kuachana na vitendo hivyo ambavyo, kwa mujibu wake, “havipendezi mbele ya Mungu na ni kinyume na maadili ya Mtanzania.
Katika hotuba hiyo, Mnzava pia aligusia athari za matumizi ya pombe kali na haramu kwa vijana, akieleza kuwa ulevi umekuwa chanzo cha kudhoofika kwa nguvu kazi ya taifa, hasa katika maeneo ya vijijini na mijini mkoani Kilimanjaro.
Aidha, alieleza kuwa ziko baadhi ya shule katika wilaya hiyo zimekosa kabisa watoto, hali iliyosababisha kufungwa kwa baadhi ya shule kutokana na upungufu mkubwa wa wanafunzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Kilimanjaro na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, Charles Mjema, alisema taifa lolote likiwa halina amani hawa watu wake hawawezi kufanya chochote kwani hata uchumi hudorora.
Akizungumzia sula la uchaguzi Askofu Charle Mjema aliwataka Watanzania kuhakikisha wanakwenda kuwachagua viongozi wenye unyenyekevu mbele za Mungu ambao wataweza kuliongoza taifa na jamii kwa ujumla.






