SERIKALI YAPIGA MARUFUKU KUTUMIA MISUMENO MNYORORO BILA KIBALI

BUNGENI-DODOMA.

Serikali imepiga marufuku matumizi ya mashine aina ya msumeno mnyororo (chain saw), kukatia miti bila kibali kutoka mamlaka husika ili kupunguza kasi ya uharibifu wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.

Aidha; imesema katika kukabiliana na janga la ukataji holela wa miti, takribani hekta milioni 5.2 za maeneo yaliyoharibiwa zinatarajiwa kupandwa miti ifikapo mwaka 2030.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi, aliyasema hayo Mei 5,2025  Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  (Muugano na Mazingira) lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini  Profesa Patrick Ndakidemi, aliyetaka kujua tamko la Serikali kwa watu wanaovuna miti kwa kutumia misumeno mnyororo (chain saw) na hivyo kuwa kikwazo katika juhudi za kuhifadhi mazingira.

Akijibu swali la Prof. Mbunge Ndakidemi, Katambi alisema kuwa pamoja na kwamba, mashine hizo zinauzwa nchini, lakini upo utaratibu maalumu unaotoa mwongozo wa kufuata ili zisitumike ovyo kwenye maeneo ambayo hayajatolewa vibali.

"Mheshimiwa Mwenyekiti kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais naomba kutoa maelekezo; Ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia chain saw bila kibali kutoka mamlaka zilizopo kwenye maeneo husika inayotambulika kisheria, kwani kuna utaratibu wa namna ya kufanya uvunaji, tunaomba wazingatie hili kwani kwa ukiukwaji wa utaratibu huu, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge Prof. Ndakidemi; aliyetaka kufahamu mpango wa serikali  wa kupanda miti kwa kipindi cha muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na janga la kukata miti.

Naibu Waziri Katabi alibainisha kuwa Serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii, inatekeleza mpango wa muda mrefu wa mkakati wa kurejesha kwa kupanda miti maeneo yaliyoharibiwa.

Naibu Waziri Katambi alisema katika mkakati huo miongoni mwa shughuli zinazoendelea ni pamoja na kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kupitia kampeni  za upandaji miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa kila mwaka.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.