MABOGINI-MOSHI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Amesema Serikali itatoa kiasi cha Sh bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chekereni–Kahe–Mabogini, yenye urefu wa kilomita 31.25, kwa kiwango cha changarawe, sambamba na ujenzi wa mitaro, madaraja pamoja na kuinua maeneo korofi.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Kilimanjaro, Waziri Mchengerwa, alisema kuwa fedha hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameridhia mradi huo ili kuboresha miundombinu ya barabara kwa wananchi wa maeneo husika.
Waziri Mchengerwa alieleza kuwa serikali pia inatafuta Sh bilioni 45 ili kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ikiwa ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuboresha miundombinu ya usafiri katika mkoa wa Kilimanjaro.
Katika ziara yake hiyo Waziri Mchengerwa aliwapongeza Wabunge wa maeneo husika Profesa Patrick Aloyce Ndakidemi (Moshi Vijijini) na Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Stephen Kimei kwa kufuatilia kwa karibu suala hilo na kuwasilisha kilio cha Wananchi Bungeni.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeendelea kuthibitisha kuwa ni Serikali sikivu na inayowajibika kwa vitendo. Tunaendelea kusikiliza na kutekeleza mahitaji ya wananchi,” alisema Waziri Mchengerwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa alitangaza kutolewa kwa Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati katika Kijiji cha Mwangaria, pamoja na Sh milioni 120 kwa ajili ya ukarabati wa shule za msingi za Mwangaria na Oria, kufuatia maombi ya Mbunge wa Vunjo, Dkt. Kimei.
Waziri alihitimisha kwa kusema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo mbalimbali kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na sekta za afya, elimu na miundombinu.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi alisema ujenzi wa barabara Spencon-Fongagate-Mabogini Chekereni hadi Kahe yenye urefu wa kilomita 31.25 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo la Mabogini lenye wakazi zaidi ya 67,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka wa 2022.
"Wakazi wa eneo hili huwa wanapata wakati mgumu haswa nyakati za mvua ambapo wengine huamua kusitisha shughuli zao za kimaendeleo", alisema.
Aidha aliipongeza Serikali kwa kuendelea kutoka fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo kwenye Jimbo la Moshi Vijijini.
"Katika kipindi cha miaka minne kwa mfano, Kata ya Mabogini imepata jumla ya Sh bilioni 8 kwa ajili ya miradi ya kimaendeleo", alisema.
Aliongeza, "Miradi hiyo ni pamoja na hospitali ya wilaya ambayo imejengwa eneo hili, ujenzi wa shule za sekondari pamoja na miradi ya maji safi na salama".









