TaCRI YAENDELEA KUBORESHA UZALISHAJI WA KAHAWA KUPITIA TEKNOLOJIA YA KURUTUBISHA UDONGO

MOSHI.

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) imeeleza kuwa inaendelea kutumia teknolojia ya kisasa ya kurutubisha udongo ili kuboresha uzalishaji wa kahawa nchini, pamoja na kukabiliana na changamoto ya wadudu waharibifu wanaoathiri zao hilo.


Mtafiti wa Udongo kutoka TaCRI, Dkt. Godsteven Maro, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi iliyofanyika Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Dkt. Maro alisema kuwa mkakati huo unalenga kuongeza tija kwa wakulima wa kahawa, hasa katika maeneo yenye udongo uliodhoofika kutokana na matumizi duni ya virutubisho, uchakavu wa ardhi, na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Kurutubisha udongo ni hatua muhimu si tu kwa kuongeza mavuno, bali pia kwa kusaidia kuondoa usumbufu katika uzalishaji wa kahawa unaotokana na wadudu waharibifu, ambao mara nyingi hujitokeza kwenye mashamba yenye udongo dhaifu," alisema Dkt. Maro.

Aidha, Dkt. Maro alibainisha kuwa TaCRI imefanikiwa kugundua aina nne mpya za miche ya kahawa ya Arabica inayovumilia ukame, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji katika maeneo yenye changamoto ya mvua hafifu au misimu mifupi ya mvua.

"Tumeweka mkazo katika utafiti wa aina ya kahawa zinazoweza kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa, na tayari aina hizo mpya zimeanza kupelekwa kwa wakulima katika baadhi ya mikoa," aliongeza.

Naye, Afisa Ubora wa Kahawa kutoka TaCRI,  Herieth Oswald, alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo, pamoja na uongezaji wa thamani wa zao la kahawa.

“Mbali na elimu ya uzalishaji wa kahawa bora, pia tunawaelimisha wakulima wa zao hili kuhusu usindikaji na masoko ili kuhakikisha kahawa yao inapata thamani kubwa zaidi sokoni, jambo ambalo husaidia kuongeza kipato chao na kuchochea uchumi wa maeneo yao,” alisema Oswald.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha usambazaji Teknolojia na Mafunzo wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa TaCRI Shelta Mseja, alisema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kupitia vituo mbalimbali vya utafiti vilivyopo katika mikoa ya Kilimanjaro, Mara, Kigoma, Ruvuma, Songwe na Kagera.

Alisema kupitia vituo hivyo, TaCRI imekuwa ikizalisha na kusambaza miche bora ya kahawa kwa wakulima kote nchini.

"Kwa msimu wa 2024/2025, TaCRI inapanga kuzalisha miche milioni 9 ya kahawa ili kukidhi mahitaji makubwa ya wakulima wanaovutiwa na miche hiyo kutokana na ubora wake na uwezo wake wa kustahimili changamoto mbalimbali za kilimo".alisema Mseja.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.