Chifu wa Marangu Frank Marealle, akiongoza kikao cha Machifu kuelekea mkutano mkuu maalum unaotarajiwa kufanyika Mei 19 mwaka huu mkoani Kilimanjaro
MOSHI.
Viongozi wa kimila zaidi ya 100 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wanatarajiwa kukutana mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu Maalum wa kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka huu.
Hayo yalisemwa Mei 4,2025 na Katibu wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Mselle, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi kuhusiana na mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Mei 19 mwaka huu katika Hoteli ya Marangu iliyoko Wilaya ya Moshi mkoani humo.
Mselle alisema mkutano huo ni jukwaa la kuwakutanisha machifu kutoka pande zote za nchi kwa lengo la kufanya maombi maalum kwa ajili ya taifa, pamoja na kupokea mawasilisho kutoka serikalini kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya uongozi wa Awamu ya Sita, ukiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Chifu Frank Marealle wa (tano) kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na machifu kutoka wilaya za mkoa wa Kilimanjaro baada ya kumalizika kwa kikao cha maandalizi ya mkutano mkuu maalu Mei 19, mwaka huu
“Katika mkutano huu viongozi wa kimila watapokea taarifa juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na serikali, sambamba na kujadili changamoto zinazozikabili jamii zetu,” alisema Mselle.
Aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye mchakato wa kidemokrasia, maombi na ushiriki wa viongozi wa kimila unatoa mchango wa kipekee katika kuimarisha amani, mshikamano na ustawi wa kitaifa.
Alisema pamoja na agenda ya maombi kwa taifa, mkutano huo pia utagusia kwa kina masuala ya mmomonyoko wa maadili katika jamii, hasa kwa watoto na vijana, sambamba na ukatili wa kijinsia unaoendelea kushuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali.
Alifafanua kwamba mkutano huo ni wa kila mwaka na hutumika kama fursa ya kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za mwaka uliopita, pamoja na kupanga mikakati ya mwaka unaofuata.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Chifu wa Marangu, Frank Marealle, alisema mkutano huo ni jukwaa la viongozi wa kimila kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo, maadili, na mwelekeo wa jamii ya Watanzania.
“Wazee wa kimila na machifu wana nafasi kubwa ya kukumbusha jamii juu ya malezi yenye misingi ya maadili, kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili, na sisi tuna jukumu la kuhakikisha watoto na vijana wanalelewa katika misingi ya mila na desturi njema,” alisema Chifu Marealle.
Aliongeza kuwa tamaduni ni kiini cha malezi bora, na ndiyo msingi wa mshikamano na maendeleo, huku akitoa pongezi kwa serikali ya Awamu ya Sita kwa kutambua mchango wa viongozi wa kimila katika kusimamia na kudumisha utambulisho wa Kitanzania.
“Tunaendelea kutambulika na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ya wajibu wetu katika kulinda na kusimamia misingi ya mila, tamaduni na maadili ya Mtanzania,” alisisitiza Chifu Marealle.
Mkutano huo pia unatarajiwa kutoa dira na maazimio yatakayosaidia si tu kuelekea uchaguzi kwa utulivu, bali pia kujenga jamii yenye maadili, mshikamano na maendeleo endelevu.

%20kutoka%20kulia%20akiwa%20katika%20picha%20ya%20pamoja%20na%20machifu%20kutoka%20wilaya%20za%20mkoa%20wa%20Kilimanjaro%20baada%20ya%20kumalizika%20kwa%20kikao%20cha%20maandalizi%20ya%20mkutano%20mkuu%20maalu%20%20Mei%2019,%20mwaka%20huu.jpg)

