WANANCHI URU KUSINI WAISHUKURU SERIKALI KUWAJENGEA KITUO CHA AFYA

URU-KUSINI

Wakazi wa Kata ya Uru Kusini halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya Uru Kusini kilichogharimu zaidi ya sh milioni 500.

Akizungumza Mkazi wa kijiji cha Longuo 'A' Catherine Kimba, ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita na Mbunge wa Jimbo la Moshi Patrick Ndakidemi kwa kuwaletea fedha za kujenga kituo cha afya katika eneo la kata yao.

"Tumepata msaada mkubwa sana kwa kuwepo kwa kwa kituo hiki kwani kimesaidia wananchi kutohangaika tena kwenda maeneo ya mbali kufuata huduma ya matibabu."alisema.

Mkazi mwingine Dominica Mayunga, alisema kabla ya ujenzi wa kituo hicho, walikuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kufuata huduma za matibabu mbali na maeneo hayo, hivyo kujengwa kwa kituo hicho kimewasaidia na kimewarahisishia kupata huduma kwa haraka.

"Serikali ya wamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetufanyia jambo kubwa sana sisi wakazi wa kata ya Uru Kusini,  kwani awali tulitegemea kupata huduma za afya kwenye zahanati,"alisema Dominica.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Christina Martine, aliishukuru serikali kuwajengea kituo hicho, huku akiendelea kuiomba serikali kupeleka gari la wagonjwa kwani ni muhimu, kuwepo katika kituo hicho ili liweze kutumika pale mgonjwa atakapopewa rufaa kwenda hospitali kubwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Naye Diwani wa kata hiyo Wilhard Kitary, aliishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo na kuwezesha kujengwa kwa kituo cha afya ndani ya kata hiyo huku akiwaomba wananchi kuyatunza majengo hayo, na watumishi kutunza vifaa vilivyopo ili vidumu kwa muda mrefu na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika kupata matibabu 

"Kituo hiki cha afya ni mkombozi mkubwa sana kwa wananchi wa kata hii, kwa kuwa kimewasaidia watu wengi hususani wanawake wajawazito kujifungua salama.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi, aliishukuru serikali kwa kuipatia halmashauri ya Moshi Vijijini zaidi ya Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya  katika kata hiyo.

Mbunge Ndakidemi; alisema huo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo katika suala zima la kupata huduma za afya na kielelezo kinachoonesha jinsi gani serikali imekuwa bega kwa bega  na wananchi wake kuhakikisha hawatembei umbali mrefu kupata huduma hiyo muhimu.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.