MWANGA-KILIMANJARO
Shule ya Sekondari ya Mwanga iliyopo katika halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, inatarajia kuanza kutumia Nishati ya Gesi ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono mikakati ya serikali ya kulinda na kuhifadhi mazingira.
Hayo yalisemwa Aprili 12,2025 na Mkuu wa shule ya sekondari hiyo Mena Kengera, wakati akisoma taarifa ya mahafali ya 16 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo alisema kuwa matumizi ya gesi badala ya kuni yatasaidia kupunguza ukataji wa miti hovyo, sambamba na kuboresha afya za wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo.
Alisema shule hiyo imekuwa ikitumia matumizi ya kuni kama nishati ya kupikia kwa muda mrefu, ambayo si rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla, hivyo wanatazamia kuanza kutumia nishati ya gesi.
Alisema matumizi ya nishati gesi yatachangia kwa kiasi kikubwa utunzaji wa mazingira ambapo kwa mwezi shule hiyo hutumia malori kati ya saba hadi nne ya kuni yenye thamani ya shilingi milioni 3.2 kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kuni na kwamba mradi huo ni sehemu ya dhamira ya shule katika kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nisafi safi, hasa katika taasisi za umma kama shule.
Akizungumza mdau wa wadau wa mazingira Daniel Mvungi alipongeza hatua ya shule hiyo kuanza kutumia nishati ya gesi huku akisema kuwa ikiwa shule nyingi zitafuata mfano wa shule ya sekondari ya Mwanga, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake mwalimu wa shule hiyo Viscud Haroun Mtarishi, alisema kuwa matumizi ya gesi yatasaidia kupunguza madhara ya kiafya kwa wapishi na wanafunzi, lakini pia yatapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni, na hivyo kusaidia juhudi za kitaifa za kuhifadhi mazingira.
"Matumizi ya gesi yanafaida nyingi zikiwemo kupika kwa haraka, usafi wa mazingira jikoni, kupungua kwa magonjwa ya njia ya upumuaji, na kuokoa muda ambao ungeweza kutumika kukusanya kuni au kusubiri kuni kushika moto.
Akiongea katika hafla hiyo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara Tours Frida Mberesero, aliupongeza uamuzi wa shule hiyo wa kwenda kuanza kutumia nishati gesi, ikiwa ni hatu za kuunga mkono juhudi za serikali za kulinda mazingira kwa kutumia nishati safi na salama.
"Katika kuunga mkono uamuzi huo, Frida aliahidi kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha nakisi ya gharama za kuutekeleza mradi huo zinapatikana ili waweze kutekeleza mradi huo mapema iwezekanavyo."alisema
Katika mahafali hiyo, jumla ya wanafunzi 54 walihitimu elimu ya kidato cha sita, ambapo kati yao wavukana walikuwa ni 32 na wasichana 22.



.jpg)




.jpg)




