MOSHI-KILIMANJARO.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, ametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bi. Mwajuma Nasombe, Kamati ya Afya na Mazingira, pamoja na Watumishi wote wa sekta ya afya kwa juhudi kubwa wanazofanya kuhakikisha mji wa Moshi unaendelea kuwa safi na salama kwa wakazi wake.
Pongezi hizo alizitoa Aprili 9,2025 wakati hafla ya kukabidhi Tuzo ya Ushindi iliyotolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.
Swai alisema juhudi hizo zimeifanya Manispaa ya Moshi kuwa mfano wa kuigwa Kitaifa katika masuala ya usafi wa mazingira, hafla hiyo pia ilihusisha uzinduzi wa gari jipya la kukusanyia taka, lililonunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Manispaa ya Moshi.
“Tuna kila sababu ya kuwapongeza watumishi wetu kwa kazi nzuri wanayoifanya kila siku, mji wetu unaendelea kuvutia kutokana na jitihada zenu,” alisema Swai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Nasombe alieleza kuwa gari hilo jipya litasaidia kuboresha huduma za ukusanyaji taka na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira.














