MSALABA MWEKUNDU WASAIDIA WAGONJWA WA TB KIBONG’OTO

KIBONG’OTO-SIHA.

CHAMA cha Msalaba Mwekundu Tanzania mkoa wa Kilimanjaro, kimeonyesha mfano mzuri wa huruma na mshikamano kwa kutoa msaada kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu, wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali Maalumu ya Taifa ya Magaonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH).

Msaada huo unahusisha sabuni kuogea na kufulia, dawa za miswaki, na mafuta ya kujipaka vyote vikiwa na thamani ya Sh laki sita.

Mratibu wa Chama hicho mkoa wa Kilimanjaro, Mohamed Kisima, alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya juhudi za kuonyesha matendo ya huruma kwa jamii.

Alisema wamekuja katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa misaada kwa wagonjwa wa kifua kikuu ikiwa ni sehemu ya kuonesha matendo ya huruma kwa wagonjwa hao kwani ni muhimu kwa jamii kusaidiana hasa katika nyakati kama hizo.

Aidha alisema chama hicho kinatarajia kuadhimisha siku ya Msalaba Mwekundu Tanzania ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika Mei 10 mwaka huu jijini Dodoma.

Akipokea msaada huo Afisa Muuguzi wa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magaonjwa Ambukizi Kibong’oto Sarah Mtoi, alikishukuru chama hicho  kwa kutambua mahitaji ya wagonjwa na kutoa misaada hiyo, akisema kuwa ni faraja kubwa kwa wagonjwa kuona jamii ikiwajali.

Nao baadhi ya wagonjwa hao akiwemo Esther Daniel na Yohana Mbwana, walitoa shukrani zao za dhati kwa misaada hiyo, huku wakijtaja misaada waliyopokea kama zawadi muhimu kwa ajili ya ustawi wao.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.