MOSHI-KILIMANJARO.
Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, umesema moja ya mafanikio ambayo yameibeba Manispaa hiyo na kuongoza kwa usafi wa mazingira nchini, ni uwepo wa sheria ndogo iliyoainisha viwango vya kulipia ada ya taka kwenye maeneo mbalimbali kama vile taasisi, viwanda, kaya na maeneo ya biashara.
Mbali na Manispaa hiyo kushika nafasi ya kwanza kwa usafi wa mazingira nchini, Mtaa wa Rengua uliopo Kata ya Mawenzi katika Manispaa ya Moshi umeibuka kuwa mtaa msafi zaidi ya mitaa yote iliyopo hapa nchini ukishika nafasi ya kwanza.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Abbas Nasombe, aliyasema hayo Aprili 9,2025 wakati wa hafla fupi ya kukabidhi tuzo za ushindi kwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, pamoja na uzinduzi wa gari jipya la kukusanyia taka lililonunuliwa na Manispaa hiyo kwa mapato yake ya ndani.
Alisema moja ya vitu vilivyoiwezesha Manispaa hiyo kushika nafasi ya kwanza kwa usafi wa mazingira nchini ni uwepo wa sheria ndogo inayoainisha viwango vya kulipia ada ya taka kwenye maeneo mbalimbali kama vile taasisi, viwanda, kaya na maeneo ya biashara.
“Mafanikio haya yametokana na mikakati ambayo tulijiwekea ya kuhakikisha mji wa Moshi unakuwa msafi kipindi chote cha mwaka”.alisema.
Alitaja mikakati mingine ni pamoja na kuongeza magari ya kuzolea taka ili kuhakikisha ufanisi katika huduma za kuzoa taka, utenganishaji taka, ubunifu wa michakato ya kuchakata taka pamoja na kuongeza uelewa kwa wakazi wa Manispaa juu ya umuhimu wa kusafisha mazingira ya kijiografia wanayoishi.
Akiongea katika hafla hiyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema kuwa ushindi huo ni heshima kubwa kwa wananchi wa halmashauri hiyo ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwa uongozi wa halmashauri hiyo linapokuja swala la usafi wa mazingira.
Aidha Mstahiki Meya alitoa pongezi zake za dhati kwa vijana wanaozunguka na magari ya kuzoa taka na kuwazawadia kiasi cha shilingi milioni 1 ili waweze kugawana na madereva wao.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliipongeza halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kwa kushika nafasi ya kwanza kama mji safi kuliko yote hapa Tanzania huku akiwataka viongozi na watumishi wote wa halmashauri hiyo kuendelea kujituma ili kulinda heshima waliyoipata.







