MOSHI-KILIMANJARO
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Dkt. Maduhu Kazi, amewataka Watumishi wa Idra ya Uhamiaji kuongeza
jitihada katika ukusanyaji mapato yatokanayo na viza kwa wageni wanaoingia
nchini , ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza mapato ya Taifa.
Dk. Kazi alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi wakati wa
ufunguzi wa kikao cha 18 cha Baraza la Wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji (TUGHE)
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji
(TRITA) mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katika hotuba yake Dkt. Kazi alisema licha ya jukumu
walilopewa Idara ya Uhamiaji ya kulinda mipaka ya nchi pamoja na vipenyo
mbalimbali, bado wana wajibu wa kuhakikisha mapato yote yatokanayo na utoaji wa viza kwa wageni yanakusanywa kimalifu.
"Ni kweli kazi yenu kubwa ni kulinda mipaka ya nchi,
lakini pia mnalo jukumu la msingi la kuhakikisha mapato ya serikali
yanapatikana kupitia ada za viza kwani
hili ni eneo muhimu sana ambalo haliwezi kubezwa,"alisema Dkt. Kazi.
Aliongeza kuwa mapato hayo ni sehemu ya ya vyanzo vya
ndani vinavyoiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake mbalimbali ya
kuwahudumia wananchi, hivvyo ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anatekeleza
jukumu hilo kwa weledi na uzalendo.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini Dkt. Anna Makakala, alisema lengo la kikao
hicho cha 18 cha Baraza la Wafanyakazi Tawi la Uhamiaji, ni kujadili
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025 na kupitisha bajeti ya mwaka
2025/2026.
"Tuna mshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan maoteo
ya bajeti ya mwaka 2024/2025 tumeyona, kumekuwa na maboresho makubwa sana kwani
hata bajeti imeongezeka ,"alisema Dkt. Makakala.
Dkt. Makakala alitoa wito kwa bajeti mpya kuzingatia
maslahi ya wafanyakazi ili waweze kutekeleza majuikumu yao kwa ufanisi, huku
akisisitiza umuhimu wa watumishi kutimiza wajibu wao ipasavyo wanapodai maslahi yao.
Aidha Kamishna Jenerali DKt. Makakala, alieleza kuwa
ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika mchakato wa bajeti ni muhimu, hasa katika
kuelekea Bunge la bajeti la mwaka 2025/2026 ili kuhakikisha mchango wao
unazingatiwa.
Naye Mwenyekiti wa (TUGHE) Taifa Joel Kaminyonge, alisema
kikao hicho kimelenga kupitia utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo na
changamoto zilizopo pamoja na kutoa mapendekezo ya maboresho katika utendaji
kazi.
"Tutapitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na kuhakikisha bajeti ijayo inajibu changamoto zilizopo kwa watumishi,"alisema.










