MOSHI-KILIMANJARO
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kupitia Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Esther Maleko, ametekeleza ahadi yake kwa Wanawake wa mkoa
huo kwa kuwakabidhi mashine 169 za kutotoleshea vifaranga vya kuku
(incubators), zenye thamani ya shilingi milioni 84.5, kwa kata zote za Mkoa wa
Kilimanjaro.
Akizungumza jana katika hafla ya kukabidhi mashine hizo, Malleko
alisema lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha wanawake kuinuka kiuchumi
kupitia shughuli za ufugaji, kuimarisha lishe katika familia, na kupunguza
utegemezi wa mikopo isiyo rafiki kwa wanawake.
Mbali na mashine hizo, Maleko aliahidi pia kutoa mitaji ya
mayai kwa ajili ya kuanzisha miradi hiyo pamoja na kupeleka wataalamu katika
kila kata ili kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya incubators, ufugaji bora wa
kuku, na usimamizi wa fedha.
Aidha, Mbunge huyo alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia mkoa wa Kilimanjaro zaidi ya Sh Trilioni 1.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali, barabara, madarasa, na mradi mkubwa wa maji wa Same–Mwanga–Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, alipongeza utekelezaji wa ahadi hiyo na kuwasihi Wanawake kuvitumia vifaa hivyo kwa tija ili kuleta maendeleo ya kweli katika jamii.
Nao baadhi ya wanufaika wa mashine hizo akiwemo Mwenyekiti wa UWT Moshi Mjini Teddy Komba; alisema wamepokea msaada huo kwa shukrani na matumaini makubwa, wakieleza kuwa sasa wataweza kupata vifaranga kwa gharama nafuu na kwa wingi, hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa kuku wa kienyeji na wa kisasa.



