MOSHI-KILIMANJARO
Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 63 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (RED CROSS) ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro imetangaza mpango wake wa kwenda kutoa misaada ya kibinadamu kwa wazee wanaoishi katika kambi ya wazee ya Njoro ikiwa ni sehemu ya kuendeleza kauli Mbiu ya Mwaka huu isemayo "Dumisha Ubinadamu"
Akizungumza na Waandishi wa habri mjini Moshi, Mratibu wa Red Cross mkoa wa Kilimanjaro, Mohamed Kisima, alisema kuwa shughuli hiyo ya kutoa misaada itafanyika Aprili 19 mwaka huu kabla ya maadhimisho ya Kitaifa yatakayofanyika Mei 10 mwaka huu Jijini Dodoma.
"Kama shirika tumejikita katika kusaidia makundi maalum ya kijamii yanayohitaji msaada wa karibu, wazee ni miongoni mwa makundi hayo na kupitia tukio hili tutatoa misaada kama mchele, sabuni za kuogea na kufulia, mafuta ya kupikia, miswaki na dawa za meno."alisema.
Aliongeza kuwa Red Cross inatambua changamoto zinazo wakabili wazee katika kambi hiyo, wengi wao wakiwa wameachwa bila msaada wa kifamilia, na hivyo shirika linachukua jukumu la kutoa faraja na matumaini kwao.
Mkazi wa kata ya Majengo halmashauri ya Manispaa ya Moshi Daniel Mvungi, alisema kitendo cha Red Cross kwenda kufanya usafi katika kambi hiyo ya wazee na kutoa misaada ya kibinadamu inatakiwa kuungwa mkono na kila taasisi, huku akisema kuwa Red Cross imeonyesha mfano wa kuigwa kwa kwenda kutoa msaada kwa kundi ambalo mara nyingi husaulika.
"Kwa kweli tunawapongeza Red Cross, hawa wazee wanahitaji sana msaada wa karibu na hisia ya kupendwa, jambo hili linaonyesha kuwa bado kuna watu wanaowajali, "alisema Mvungi.
Naye Mwalimu Japhet Mpande Mkazi wa Pasua alisema "Nimefarijika kusikia kwa wazee wa Njoro watapatiwa misaada , sisi wazee tunahitaji kutunzwa na kuthaminiwa , hongera sana Red Cross kwa moyo huo wa kibinadamu.
"Tendo la Red Cross kwenda kuwatembelea wazee na kuwapatia misaada ya kibinadamu linatakiwa kupongezwa na kila mmoja,wale wazee kufikiwa na wageni mara kwa mara kunawapa faraja kubwa sana, kunawaongezea uzuri wa maisha na faraja ya moyo."alisema.
Red Cross imekuwa mstari wa mbele katika kutoa misaada ya dharura, huduma za afya, elimu ya majanga na matendo ya huruma katika jamii mbalimbali nchini , maadhimisho ya miaka 63 yanatarajiwa kukutanisha wanachama kutoka mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.




