MDAU WA UTALII WILAYA YA MWANGA AISHAURI SERIKALI KUJENGA CHUO CHA UTALII

MWANGA-KILIMANJARO.

Mdau wa masuala ya utalii Wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro Frida Mberesero, ametoa wito kwa serikali kuanzisha Chuo cha Utalii katika wilaya hiyo ili kuwawezesha vijana wa eneo hilo kupata  elimu na mafunzo ya kitaalamu katika sekta ya utalii.

Mberesero alitoa ushauri huo Aprili 12,2025 akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 16 ya wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2025 shule ya sekondari Mwanga, inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania.

Mberesero alisema kuwa vijana wengi wanaohitimu elimu ya sekondari na vyuo vya kati wanakosa fursa ya kujiendeleza katika kozi za utalii, jambo linalopelekea uagizwaji wa
waongoza watalii kutoka Jijini Arusha na Moshi mjini.

"Waongoza watalii kutoka nje ya Mwanga hawana uelewa wa kutosha kuhusu jiografia, historia na vivutio vya kipekee vilivyopo katika wilaya yetu, vijana wetu wana maarifa ya ndani  na ari kubwa, wakipewa mafunzo rasmi wataweza kufanya kazi hii kwa weledi na kuongeza kipato chao,"alisema.


Aidha; alibainisha kuwa uanzishwaji wa chuo hicho utasaidia kukuza uchumi wa wilaya kwa kuongeza ajira, kupunguza wimbi la wahitimu wasio na ajira  na kuimarisha ushiriki wa jamii katika shughuli za utalii wa ndani.

"Tunayo maliasili nyingi, mandhari ya kuvutia  na vivutio  vya kihistoria ambavyo bado havijatumiwa ipasavyo kwa kuwajengea vijana wetu uwezo kupitia elimu ya utalii tutakuwa tumefungua milango ya maendeleo ya kweli kwa wilaya ya Mwanga ,"aliongeza.

Wito huo ulipokelewa kwa shangwe na wazazi, walimu na wahitimu wa shule hiyo, huku wengi wao wakieleza kuwa ni hatua ambayo italeta mabadiliko chanya katika maisha ya vijana na maendeleo ya Wilaya hiyo kwa ujumla.

Nguluma Kajoto, mzazi wa mmoja wa wahitimu alisema;  "Tumekuwa tukishuhudia vijana wetu wakihitimu na kukaa nyumbani kwa kukosa fursa sahihi, chuo cha utalii kitakuwa mkombozi mkubwa, kwani wilaya ya Mwanga tuna vivutio vingi lakini hatuna wataalamu kutoka kwetu wenyewe."alisema.

Kwa upande wake Victoria Swai na Prosper Mathias Kwandilile, miongoni mwa wahitimu wa kidato cha sita walisema; "Wangependa sana kusomea masuala ya utalii, kujengwa chuo cha utalii hapa Mwanga kitatusaidia sisi vijana wa hapa kujifunza na kujiajiri."walisema.

Naye Katibu wa UWT Wilaya ya Mwanga Cesilia Ismail, aliishauri serikali kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha wazo hilo linatimizwa kwa vitendo huku akisisitiza kuwa Mwanga ina kila sababu ya kuwa kitovu cha utalii wa ndani.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.