Serikali imemuelekeza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kufanya tathmini katika zahanati ya Shia iliyopo kata ya Kimochi ili kuona kama inafaa kupandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya.
Maelekezo hayo yametolewa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi.
Katika Swali lake Mbunge Ndakidemi aliuliza ni lini Serikali itaipandisha hadhi Zahanati ya Shia ili kuwa kituo cha afya ili kuunga mkono juhudi za wananchi wa eneo hilo.
"Nashukuru sana Mhe; Mwenyekiti kwa kunipa nafasi ya kuuliza Swali la nyongeza; Wananchi wa kata ya Kimochi wana hamu kubwa sana ya kupandishwa zahanati ya Shia ili kuwa kituo cha afya Je? Serikali iko tayari kusaidia wananchi hao kufikia azma yao hiyo?Akijibu Swali hilo Naibu Waziri Dugange alisema Serikali inautaratibu wake wa kupandisha hadhi zahanati na kuwa kituo cha afya kwa kuangalia idadi ya watu pamoja na ukubwa wa eneo lililopo.
Alisema kama serikali ilisha weka kwa kila zahanati ambapo menejimenti ya wilaya inaona kama kuna sababu ya kuipandisha hadhi kuwa kituo cha afya.
"Kuna utaratibu ambao wanatakiwa kuufuata, naomba nitumia nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Moshi kufanya tathmini kwenye zahanati ya Shia kwa maana ya kupata idadi ya wananchi waliopo, lakini pia ukubwa wa eneo na kuleta maombi ya kuipandisha hadi zahanati hiyo ili kuwa kituo cha afya, ili serikali iweze kufanya tathmini na kutenga fedha kuafikiana na halmashauri na serikali kuu kwa ajili ya kuipandisha hadhi."


