MOSHI-KILIMANJARO.
Timu ya waendesha baiskeli 12 inatarajia kuanza safari ya kipekee kupitia mbuga ya wanyama ya Saadani, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani na wa kimataifa kwa kutumia baiskeli kama chombo cha kutangaza vivutio vya asili vya Tanzania.
Safari hiyo, inayojulikana kama "Kili Red Bickers 2025," imeandaliwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (RED CROSS) Tawi la Mkoa wa Kilimanjaro.
Safari ya waendesha baiskeli hao itaanza Mei Mosi Mwaka huu, ambapo watapitia njia ya kipekee inayokatiza pori la Saadani hadi ufukwe wa Bahari ya Hindi, wakileta pamoja uzuri wa wanyama pori na mandhari ya fukwe.
"Tumewaita hapa leo hii kufanya utambulisho rasmi wa timu ya waendesha baiskeli 12 ambao wataongoza uhamasishaji wa wanancha na voluntia wa Red Cross kushiriki kwa wingi kwenye maadhimisho ya Siku ya Red Cross Duniani ambayo yatafanyika Mei 10 mwaka huu, yatakwenda sambamaba na kuadhimisha miaka 63 ya Tanzania Red Cross Society, Maadhimisho ambayo yatafanyika Mkoani Dodoma."alisema Kisima.
Kisima alisema kwenye timu ya waendesha baiskeli ina Wanaume 11 na Mwanamke mmoja ambapo kwenye safari hiyo kuelekea Dodoma watapeperusha bendera ya Red Cross kwa siku 10 kwa kuendesha kilometa 1027 kutoka Kilimanjaro hadi Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Red Cross mkoa wa Kilimanjaro Mohamed Omary Kisima, alisema safari hiyo inalenga kuonesha namna ambavyo utalii endelevu unaweza kufanyika kwa kutumia baiskeli, kama chombo rafiki kwa mazingira, kinachotoa nafasi kwa wageni kuungana moja kwa moja na uzuri wa Tanzania.