MWANAMKE PEKEE WA KILI RED BICKERS KUENDESHA BAISKELI KILOMETA 1,027 KUTOKA KILIMANJARO HADI DODOMA


MALKIA WA KILI RED BIKERS LILIANI JOSEPH KITHII (23), ATAKAYEVUKA KILIMANJARO HADI DODOMA KWA BAISKELI

MOSHI

Katika kundi la waendesha baiskeli 12 wanaojitayarisha kwa safari ya kihistoria kutoka Kilimanjaro hadi Dodoma, yupo mrembo mmoja jasiri Liliani Joseph Kithii, mwenye umri wa miaka 23, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kikosi cha Red Kili Biker.

Safari hiyo ya zaidi ya kilomita 1,027 inalenga kutangaza utalii wa ndani, kuhamasisha shughuli za Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na mazingira.

Katika mahojiano mafupi, Liliani anafunguka kuhusu safari yake ya ndoto, mapenzi yake kwa baiskeli, na matumaini yake kama binti wa Kitanzania.

MAHOJIANO:

Mwandishi: Liliani, hongera kwa kuwa sehemu ya safari hii ya kipekee; Unajisikiaje kuwa mwanamke pekee kwenye timu?

Liliani Kithii:

Nashukuru sana; Mimi ni miongoni mwa waendesha baiskeli pekee kwenye timu hii ya watu 12, na ni heshima kubwa kuwa sehemu ya safari hii, najivunia kuwa mwanamke pekee, si kwa kushindana, bali kuonyesha kuwa tunaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaifa, hasa zile zinazohusisha afya, utalii na mazingira.

Mwandishi: Ulianza lini kupenda baiskeli?

Liliani:

Nikiwa na umri mdogo, nilikuwa napenda sana kuendesha baiskeli, ilikuwa sehemu ya maisha yangu ya kila siku. Wakati wenzangu walicheza michezo mingine, mimi nilichagua baiskeli. 

Na leo hii, hiyo ndoto ya utotoni inaniongoza hadi kwenye safari hii kubwa zaidi maishani mwangu.

Mwandishi: Safari hii inapitia Hifadhi ya Taifa ya Saadani; hilo lina maana gani kwako?

Liliani:

Kupita katika Mbuga ya Saadani ni fursa ya kipekee, ni hifadhi pekee Barani Afrika inayokutanisha wanyamapori na bahari katika eneo moja.

"Kwangu mimi hii ni nafasi ya kuutangaza utalii wetu kupitia Red Kili Bikers,naamini kupitia macho yetu na njia tunazopita, tutaibeba Tanzania kwa namna ya tofauti kabisa.

Mwandishi: Unatumaini nini baada ya safari hii?

Liliani:

Natumaini kuwa wanawake wengi watahamasika kushiriki kwenye shughuli kama hizi,na pia watambue kuwa utalii sio wa wageni pekee.

"Sisi Watanzania tuna kila sababu ya kuuishi, kuutembelea na kuutangaza, niko hapa kama sauti ya mabinti wenzangu kuwa tunaweza kuvunja mipaka kwa miguu miwili na moyo mmoja.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.