MBUNGE WA JIMBO LA VUNJO DKT. CHARLES KIMEI, ATAJWA KAMA KIONGOZI ANAYEJALI MAENDELEO YA WANANCHI WAKE

VUNJO-KILIMANJARO

Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro  Dkt. Charles Kimei, ametajwa kama kiongozi anayejali maendeleo ya wananchi wake, huku wakisisitiza kuwa uwakilishi wake umejikita katika kutatua changamoto zinazowakumba wananchi kwa vitendo.

Akiwaongoza wananchi wake kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kasi, Dkt. Kimei amekuwa mfano wa uwajibikaji na kujitolea katika kuhakikisha kwamba jimbo lake linapata maendeleo endelevu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti  baadhi ya wananchi kutoka kata nane za jimbo la Vunjo mkoani humo, wamesifu juhudi za Mbunge huyo, wakisema kwamba ameleta mabadiliko makubwa kwa kuzingatia mahitaji yao ya kimsingi.

Mkazi wa Kata ya Marangu Mashariki Rosemary Mosha alisema, "Mbunge wetu ameonesha tofauti kubwa na  Wabunge waliomtangulia, yupo jimboni mara kwa mara na anasimamia miradi kwa karibu, jambo ambalo halikuwa linaonekana hapo awali."alisema Bi. Rosemary.

Alisema Mbunge Dkt. Kimei ameleta mabadiliko makubwwa hususani kwenye sekta ya miundombinu ya barabara, afya, elimu, na maji, huku akitolea mfano kwenye daraja linalounganisha vijiji vya Sembeti na Samanga ambapo limeboreshwa huku daraja la Marangu Mtoni likipanuliwa.

Mkazi mwingine wa kata hiyo Richard Kawiche, alieleza kwamba Dkt. Kimei alianzisha miradi mbalimbali ya elimu na maji, akitoa Sh milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Sakayo Mosha, pamoja na Sh milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko cha Mshiri.

Kiwiche aliongeza kusema kuwa  mradi mwingine ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Marangu Hedikota ni miongoni mwa mafanikio yaliyoshuhudiwa.

Vilevile, aliongeza kusema kuwa Mbunge Kimei, alichangia madawati 50 kwa Sekondari ya Ashira, na sasa jimbo hilo lina mradi mkubwa wa maji wa Sh milioni 346 unaotekelezwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).

Naye Hardson Mmanyi  mkazi wa Kahe Mashariki alisema, "Tunampongeza Mbunge Dkt. Kimei na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri wanazofanya. 

"Tumeona mabadiliko ya kweli katika kata yetu, kama vile barabara ya Papliki–Majengo–Kochakindo na huduma ya umeme kwa vijiji ambavyo vilikuwa vikiwa gizani."

Ally Msangi kutoka Makuyuni alisema, "Vunjo ilikuwa ni jimbo la siasa za msimu, lakini sasa tunaona mabadiliko halisi Dkt. Kimei ni kiongozi wa mfano na tunapaswa kuendelea kumuunga mkono ili aendelee kutimiza ahadi za maendeleo."

Kwa upande wake Diwani wa Makuyuni, Dickson Tarimo, alisema "Kata ya Makuyuni imepokea miradi mingi ya maendeleo kutoka kwa Mbunge wetu, Dkt. Kimei, na Rais Samia Suluhu Hassan, hatuwezi kujizuia kuwapa kura za kutosha kwa sababu ya kazi nzuri wanazozifanya."

Jimbo la Vunjo linaundwa na Kata za Marangu Mashariki, Njiapanda, Kahe Mashariki, Kirua Vunjo Kusini, Kilema Kusini, Kirua Vunjo Mashariki, Makuyuni, na Kirua Vunjo Magharibi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.