VUNJO-KILIMANJARO
Madiwani wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro wamepongeza juhudi kubwa za Mbunge wao, Dkt. Charles Kimei, huku wakieleza kuwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata zao imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi.
Huku baadhi ya madiwani wakimtaja Mbunge Dkt. Charles Kimei si tu kiongozi wa kisiasa, bali pia kiongozi mwenye juhudi za kipekee katika kuboresha huduma za jamii.
KAZI ZA MBUNGE DKT. KIMEI KATIKA KATA YA MAKUYUNI
Akizungumzia maendeleo ya Kata yake Diwani wa Kata ya Makuyuni, Dickson Tarimo, alisema "Kata yetu imepokea miradi mingi ya maendeleo tangu Dkt. Kimei kuingia madarakani.
"Kwa kazi nzuri ambazo zimeonekana kwa vitendo, tunapaswa kumsaidia kwa kumpa kura za kutosha ili aendelee kutekeleza miradi hii katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo."alisema Tarimo.
Aidha Diwani Tarimo alitaja baadhi ya miradi muhimu iliyoonyeshwa katika kata yhiyo, ni pamoja na shule ya Sekondari Himo ambayo imepokea miundombinu ya kidato cha 5 na 6, na kwamba kituo cha wagonjwa wa nje (OPD) Himo kimepandishwa hadhi kuwa kituo kamili cha afya.
Aliongeza kuwa maboresho makubwa ya huduma za afya yamefanyika, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya afya ya uzazi na watoto, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 74, pamoja na ujenzi wa madarasa na ununuzi wa madawati katika shule za msingi na sekondari.
KAZI ZA MBUNGE DKT. KIMEI KATIKA KATA YA KIRUA VUNJO MAGHARIBI
Naye Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, John Kessy, alieleza mafanikio ya miradi katika kata yake, akisema, "Kituo cha Afya Kirua Vunjo kilipata fedha Sh milioni 500 kwa ajili ya upanuzi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya maabara, upasuaji, na huduma ya mama na mtoto, ambapo pia walifanikiwa kukamilisha choo cha soko la Rindima na paa la soko."
Diwani Kessy alisema miradi hiyo imeboresha mazingira ya biashara na huduma za afya katika kata hiyo, na kwamba mafanikio haya yamejidhihirisha kwa wananchi wa Kirua Vunjo Magharibi.
KAZI ZA MBUNGE KIMEI KATA YA NJIAPANDA
Kizungumza Diwani wa Kata ya Njiapanda, Loveness Mfinanga, alisema kuwa wananchi wa kata hiyo, wanamuunga mkono Dkt. Kimei si kwa sababu ni mwana-CCM pekee, bali kwa sababu amefanya kazi kubwa za kuwaletea maendeleo ambazo zinaonekana.
"Katika kata yangu, Mbunge Dkt. Kimei amefanikisha kuleta mradi mkubwa wa maji wa Sh bilioni 2.3, ambao umeondoa kabisa kero ya maji," alisema Diwani Loveness.
Alifafanua kuwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Njiapanda na zahanati mbili, pamoja na ujenzi wa shule ya msingi darajani, umeleta nafuu kubwa kwa wananchi wa kata hiyo.
"Matengenezo ya barabara za kata pia yameboreshwa, na wananchi wanashuhudia mabadiliko halisi katika huduma za kijamii.
KAZI ZA MBUNGE KIMEI KATA YA KITUA VUNJO MASHARIKI
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Alex Umbela, alisema, "Nimeshuhudia na kufanya kazi na wabunge wengi, lakini Dkt. Kimei ni wa kipekee katika utendaji wa matokeo ya haraka.
Alisema shule mbili za msingi Mrumeni na Msufini zimeshuhudia maboresho makubwa, huku zahanati mpya ya Kileuo na maboresho katika zahanati ya Nganjoni pia yakifanyika.
Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Uchira-Kisomachi-Kolarie kwa kiwango cha lami, ambayo tayari mkandarasi yupo kazini, ni mojawapo ya mifano ya miradi inayoendelea kuboresha miundombinu ya kata yake.
Akizungumza Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Kimei alisema kuwa umoja na mshikamano ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kuendelea kumsemea vizuri Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Kimei alisema "Serikali imefanya kazi kubwa ya kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025. Kazi hizi ni matokeo ya ushirikiano na ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo yao."
Matokeo ya miradi ya maendeleo yanaonekana wazi kwa wananchi, na madiwani wa Jimbo la Vunjo, wanasisitiza kuwa ili mafanikio hayo yaendelee, wananchi wanapaswa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge Dkt. Charles Kimei kwa kutoa kura zao katika uchaguzi ujao.