MOSHI-KILIMANJARO
Ndizi
ni moja ya mazao muhimu ya chakula na biashara katika Afrika Mashariki, katika
maeneo mengi ya kanda hii, ndizi hutumika kama chakula kikuu kwa familia
nyingi, na pia ni chanzo muhimu cha kipato kwa wakulima.
Katika
maeneo ya vijijini, ndizi za kupika, kama vile matoke, ni chakula cha kila
siku, ambacho huliwa kwa namna mbalimbali: kuchemshwa, kukaangwa, au kupikwa
kwa mchuzi.
Ndizi
si tu kwamba ni chakula kinachoweza kutumika kwa haraka na kwa urahisi, bali
pia ni chanzo cha lishe bora, zina kiwango cha juu cha wanga, vitamini muhimu
kama vile vitamini C, na madini kama potasiamu, ambayo ni muhimu kwa afya ya
moyo na kudhibiti shinikizo la damu.
Kwa upande wa biashara, ndizi ni zao ambalo lina mchango mkubwa kwa Wakulima, kwa wengi wao, ndizi ni chanzo kikubwa cha kipato.
Katika
kulitambua hilo Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi ametoa
miche 10,000 ya migomba kwa kata 14 zilizoko ukanda wa milimani ili kuhakikisha
zao hilo linaendelea kupatikana kwa wingi.
Hayo
aliyasema Aprili mosi, 2025 katika hafla fupi ya makabidhiano ya miche hiyo, kwa
viongozi wa CCM kutoka kata 14 za Moshi vijijini ambapo zao hilo limekuwa
likilimwa kwa kiasi kikubwa.
Prof.
Ndakideni alisema kuwa lengo la kutoa miche hiyo ni kuhamasisha uzalishaji wa
ndizi na kuongeza tija kwa wakulima wa milimani.
Alisema; kilimo cha ndizi kina manufaa makubwa katika kuboresha lishe, kuongeza kipato cha familia, na kuchangia katika uchumi wa jamii.
“Jimbo
la Moshi Vijijini hususan ukanda wa milimani una ardhi na mazingira bora kwa
kilimo cha migomba na mbegu niliyowapa itaenda kuongeza uzalishaji ambapo
mkungu mmoja unaweza kufikisha kilo 150 hadi 200 ukilinganisha na migomba
iliyopo kwa sasa ambayo wanavuna kati ya kilo 10 hadi 50.”alisema,
Aliongeza kuwa “Zao hili linachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa familia na jamii, katika baadhi ya maeneo, ndizi hufanyika kama biashara kubwa ambayo inategemea uzalishaji na usafirishaji wa ndizi kwenda katika miji mikubwa na hata nchi nyingine,”alisema Prof. Ndakidemi.
Alifafanua
kuwa wakati wa kampeni mwaka 2020 aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwaletea
migomba, ambapo aliwasiliana na taasisi ya Kimataifa ya The International
Institute of Tropical Agriculture (IITA)
ambayo ilimpatia ufadhili wa mbegu hizo kupitia kwa Profesa Rony Swenen.
Aidha
alisema kuwa Serikali inaandaa mpango maalumu utakaofanya zao la ndizi kuwa zao
la kibiashara hivyo wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo watanufaika
na miche hiyo ili ile dhima iliyokusudiwa iweze kutimia.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti mara baada ya kukabidhiwa miche hiyo baadhi ya viongozi wa
CCM katika kata hizo akiwemo Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Andrew Mwandu, Katibu
wa CCM Kata ya Mbokomu Sofia Mshiu na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Old Moshi
Mashariki Ronald Tenga walisema mbegu hizo zitasaidia wakulima kuzalisha kwa
tija na kuongeza mapato ya kaya.