UVCCM KATA YA MAKUYUNI WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO

HIMO-MAKUYUNI

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kata ya Makuyuni Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoni Kilimanjaro, umemshukuru Mwenyekiti wa (CCM) Taifa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akiguswa na changamoto zinazowakabili wananchi waishio maeneo ya pembezoni.

Shukrani hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Makuyuni Sunday Chilembwe, wakati akifungua kikao cha Baraza la UVCCM Kata hiyo kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa King Size uliopo Mji mdogo wa Himo Wilayani humo.

Alisema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan Kata hiyo imenufaika na miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja linalounganisha vitongoji vya Msufini na Kisimani Kata ya Makuyuni hali itakayowarahisishia wananchi wa maeneo hayo mawasiliano toka upande mmoja kwenda upande mwingine.

Alisema katika Sekta ya miundombinu Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara mpya ya Himo-Makuyuni-Lotima yenye urefu wa kilometa 6.6 ambayo inajengwa kwa Sh bilioni 3.6. kwa kiwango cha lami.

“Ninamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akiguswa na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata ya Makuyuni, kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake ametushushia fedha kiasi cha Sh bilioni 6.6 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Kata yetu”alisema Chilembwe.

Chilembwe; alisema katika Sekta ya elimu Kata  hiyo imenufaika kwa kupata shule ya mpya ya sekondari Himo ambayo ni ya kidato cha tano na sita iliyojengwa kwa Sh milioni 492.

“Fedha hizi zimeletwa kupitia mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania Bara (BOOSTER), ujenzi wa vyumba vya madarasa na ukarabati wa madarasa ya zamani shule za msingi na shule ya sekondari Meresini zilizopo ndani ya kata yetu,”alisema.

Kwa upande wa sekta ya afya  Chilembwe  alisema mbali na ununuzi wa  mashine ya x-ray, katika kituo cha afya Himo, ambapo serikali ilitoa kiasi cha Sh milioni 200, pia ilinunua  mtambo wa kisasa wa kung’oa na kujaza meno pamoja na ununuzi wa gari la wagonjwa katika kituo hicho.

“Katika kipindi hicho Rais Samia amefanya mambo makubwa sana ndani ya Kata ya Makuyuni ikiwemo uboreshaji wa huduma za fya, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa ongezeko la madaktari, wauguzi na upatikanaji wa dawa za kutosha katika kituo cha afya,”alisema.

Pia alisema kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia wamepata jengo jipya la huduma ya mama na mtoto  lililojengwa katika zahanati ya Makuyuni.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo alisema baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza hilo pia UVCCM Kata ya Makuyuni walifuturisha viongozi mbalimbali wakiwemo wa chama na serikali.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.