MOSHI-KILIMANJARO.
Bodi ya Maji Bonde la
Pangani (PBWB) imezitaka taasisi za kisekta zinazochukua maji kutoka vyanzo vya
maji kuhakikisha kwamba wanalipia huduma hiyo ili kuboresha usimamizi wa
rasilimali za maji
Mkurugenzi wa bodi
hiyo, Mhandisi Segule Segule, aliyasema hayo Machi 29,2025, wakati akizungumza
na wadau wa maji kwenye kikao cha mapendekezo ya majina ya Wajumbe wa Bodi ya
11 ya Maji Bonde la Pangani, mkutano uliofanyika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa
Kilimanjaro.
Katika mkutano huo, Mhandisi Segule alisisitiza umuhimu wa taasisi za kisekta zinazochukua maji kutoka vyanzo vya maji kuhakikisha wanalipia huduma ya maji, kama sehemu ya juhudi za kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji na kuhamasisha uwajibikaji katika matumizi ya maji.
Aliweka wazi kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi wa mikoa inayozungukwa na vyanzo vya maji, kwani itasaidia kudumisha usawa katika matumizi ya rasilimali hiyo adimu na kuhakikisha kuwa huduma za maji zinapatikana kwa wote.
Alisema kuwa uharibifu
wa mazingira kwenye vyanzo vya maji kwa kawaida una viashiria vingi na kwamba
vyanzo vya maji vilivyo karibu na maeneo ya miji vinakuwa kwenye hatari kubwa
zaidi, huku akisema kuwa shughuli za binadamu, kama vile kilimo, uchimbaji wa
mchanga, ujenzi na uchafuzi wa mazingira, ni miongoni mwa mambo yanayoathiri
vyanzo vya maji na kusababisha upungufu wa maji safi na salama.
“Vyanzo vya maji vilivyo karibu na miji vinapozidi kuchafuliwa na kuharibiwa, ni vigumu kudumisha ubora wa maji na viwango vya usafi vinavyohitajika kwa matumizi ya binadamu, kilimo, na viwanda na kuwataka wadau wote wa maji kuchukua hatua za pamoja katika kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa kwa manufaa ya jamii nzima”.alisema.
Alisema kuwa PBWB imejiwekea mikakati madhubuti ya kuhakikisha inatembelea maeneo yote yenye vyanzo vya maji vilivyoko mijini, kwa lengo la kuweka alama za kuzuia maendelezo mapya ya makazi ndani ya mita 60 kutoka kwa vyanzo vya maji.
“Mikakati hii inalenga
kudhibiti ujenzi holela na matumizi yasiyofaa katika maeneo muhimu ya vyanzo
vya maji, ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinatunzwa kwa manufaa ya vizazi
vijavyo,”alisema Mhandisi Segule.
Alisema kuwa watu
wengi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji, hasa katika maeneo ya mijini, mara nyingi
huathiri mazingira kwa ujenzi na shughuli nyingine zinazoharibu vyanzo vya
maji, kwa kuweka alama na kudhibiti ujenzi ndani ya umbali huo wa mita 60, Bodi
ya Maji Bonde la Pangani inatarajia kulinda vyanzo vya maji na kuboresha ubora
wa maji kwa matumizi ya jamii nzima.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Nzowa, Mhandisi Jackson Masaka kutoka sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, aliwataka wale watakaochaguliwa kuiongoza Bodi ya Maji Bonde la Pangani, kuzingatia weledi na uadilifu wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Wajunbe
watapakapokabidhiwa wajibu wa kuiongoza bodi hii, wahakikishe wanatekeleza
wajibu wao kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa raslimali za maji namba 11 ya
mwaka wa 2009,”alisema Mhandisi Masaka.
Katika kikao hicho
Mhandisi Masaka aliupongeza uongozi wa Bodi ya Maji Pangani, kwa kufanya
shughuli zake kwa kutumia dhana ya ushirikishi jambo ambalo alisema linachangia
kuweko kwa amani miongoni mwa watumia maji.
Akizungumza kwa niaba
ya Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Rasilimali za Maji, Wizara ya Maji
Modestus Zacharia, alisema kuwa rasilimali za maji zinazidi kupungua kutokana
na uwepo wa shughuli za binadamu kwenye vyanzo vya maji.