Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, akimjulia hali majeruhi wa basi la Mvungi Eliakili Juma Mvungi anayepatiwa matibau katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi.
MOSHI-KILIMANJARO.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro Joseph Tadayo, ameushukuru uongozi wa hospitali za rufaa ya Mkoa Mawenzi na ile ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMCM kwa kuwahudumia vyema majeruhi waliopata ajali basi, Wilayani Mwanga siku ya Alhamisi.
Mbunge Tadayo alitoa pongezi hizo Aprili 4,2025 mjini Moshi,
baada ya kuwatembelea na kuwajulia hali majeruhi hao wanaoendelea na matibabu
katika hospitali ya Mawenzi na KCMC.
“Niwashukuru sana viongozi wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC na uongozi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa Mawenzi, hususani madaktari, wahudumu wa afya na wauguzi kwa namna mlivyowapokea majeruhi hawa na kuwapa huduma za haraka, hili limenipa faraja na wana imani kubwa kwenu”, alisema Mbunge Tadayo.
Tadayo alisema inatia moyo kuona majeruhi hawa wanaendelea vyema, baada ya kupata huduma hizo nzuri baada ya ajali hiyo iliyotokea asubuhi ya Alhamisi.
Aidha Mbunge Tadayo alitoa pongezi kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga, Wajumbe wa Kamati ya usalama ya Wilaya ya Mwanga na Kamati ya Usalama ya mkoa wa Kilimanjaro, kwa kujitoa kwa hali na mali wakati ajali hiyo ilipotokea jambo ambalo alisema imeonyesha mshikamano walionao wananchi wa wilaya ya Mwanga.
Katika hatua nyingine Mbunge Tadayo, alitoa rai kwa wale wote wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini wakati wa kipindi hiki cha mvua kwani maeneo mengi ya milimani licha ya kuwa ni barabara ya lami lakini kuna utelezi.
“Sasa hivi ni kipindi cha mvua, maeneo mengi kwa sasa haswa yale ya milimani yana utelezi, hivyo ni vyema wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini ili kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea”, alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya KCMC Dk. Sarah Urassa, alimshukuru Mbunge Tadayo kwa kuweza kufika na kuwajulia hali majeruhi hao.“Tumepokea ugeni wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tasdayo, ambaye alifika hapa kwa ajili ya kuwajulia hali majeruhi wa ajili iliyotokea kwenye jimbo lake,”alisema.
Pia Dk. Urassa; alitoa rai kwa wataalam wa afya kuhakikisha kwamba kuna kuweko na wataalam kwenye magari ya wagonjwa ambayo husafirishia wagonjwa mbalimbali wakiwemo majeruhi, jambo ambalo litasaidia kuokoa maisha ya watu wengi kwa vile wataalam hao watakuwa wanaendelea kuwapa huduma za awali wakati wakiwa njiani majeruhi hao kuletwa hospitali ya rufaa.
“Hili litasaidia kuokoa maisha ya watu wengi kwa vile wataalam hawa watakuwa wanaendelea kuwapa huduma za awali wakati wakiwa njiani kuletwa hospitali ya rufaa”, alisema Dk. Urasssa.
Naye Kaimu Mganga Mafawidhi hospitali ya rufaa ya Mkoa Mawenzi Dk. Jackline Malyi, alisema kuwa majeruhi 24 walipokelewa hospitalini hapo na kati yao hao 18 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka ambapo sita bado wanaendelea na matibabu huku mmoja wao akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututii.
“Kati yao hao 18 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka ambapo sita bado wanaendelea na matibabu huku mmoja wao akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi”, alisema Dk. Malyi.
Nao baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo Harun Selemani, Eliakili Juma Mvungi na dereva wa basi Ladani Hamis Mruma, waliwapongeza wahudumu wa afya katika hospitali hizo kwa jinsi walivyowashughulikia kwa haraka jambo ambalo limepelekea kupata unafuu.
Vile vile majeruhi hao “wamempongeza Mbunge Tadayo kwa kuja kuwajulia hali jambo ambalo walisema limewapa faraja kubwa kwao,”walisema.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (SACP) Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
SACP Maigwa alisema ajali hiyo ilitokea Alhamisi ya Aprili
3,2025 majira ya saa moja asubuhi, eneo
la Kikweni Kijiji cha Mamba, Wilaya ya Mwanga, mkioani humo ambapo basi la
Kampuni ya Mvungi, lilikuwa likitokea Ugweno kuelekea Jijini Dar es Salaam,
liliacha njia na kupindukia kwenye bonde na kusababisha vifo vya watu saba,
wanaume wawili na wanawake tano”, alisema.