CCM YATUMA SALAMU ZA POLE KWA FAMILIA YA KATIBU MWENEZI WA CCM KATA YA MAWENZI MAREHEMU RUTH NEVATI KAZOKA


MAWENZI-MOSHI.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mawenzi, Wilaya ya Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro, Joanith John Byarushengo, ametuma salamu za pole kwa familia ya marehemu Ruth Nevati Kazoka, Katibu Mwenezi wa CCM Kata hiyo, ambaye alifariki dunia Aprili 4, 2025, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC, kutokana na tatizo la moyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Aprli 5,2025, Byarushengo alielezea masikitiko na huzuni yake kwa kupokea taarifa za kifo cha Kazoka, ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu na mwanachama shupavu wa CCM.

Alisema marehemu Kazoka alikuwa mfano wa kujitolea na alikuwa na mapenzi makubwa kwa chama chake, ambaye aliweza kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi wa 2015, katika Jimbo la Kawe ambapo alifanya kazi kwa bidii na kwa ari kubwa.

Byarushengo; alisema kuwa Uchaguzi wa mwaka 2015 wa Rais, Wabunge na Madiwani, marehemu akiwa mwanachama wa kawaida, alishiriki kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kippi Warioba.

"Marehemu Kazoka alifanya kampeni kwa namna ya kipekee, utadhani alikuwa kiongozi, kutokana na namna alivyokuwa anapigania chama chake, alikuwa na roho ya kujitolea na utumishi kwa chama na taifa lake," alisema Byarushengo.

Aidha, Byarushengo alikumbuka mchango wa Kazoka katika uchaguzi wa ndani ya chama mwaka 2022, ambapo aligombea nafasi ya Katibu Mwenezi ngazi ya Tawi la Hindu, na ingawa hakufanikiwa, alikubali kushindwa kwa heshima na alijitokeza tena kugombea nafasi ya Katibu Mwenezi ngazi ya Kata na kufanikiwa kushinda.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, alielezea hisia zake za huzuni kwa kumpoteza Ruth Kazoka, akimkumbuka kwa utii, uaminifu, na uzalendo wake katika utumishi wake kwa chama na taifa.

"Napenda kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, Ndugu, Jamaa, Wanachama wa CCM, na Watanzania wote walioguswa na msiba huu mkubwa," alisema Diwani Naburi.

Marehemu Ruth Nevati Kazoka atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika chama na jamii kwa ujumla.

"Bwana alitoa na Bwana ametwaa Jina lake libarikiwe."

AMEN.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.