SAME-KILIMANJARO
Vijana wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia nne inayotolewa na serikali kupitia halmashauri ili kujikwamua kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ile ya kilimo na ufugaji.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (MNEC), kupitia mkoa wa Kilimanjaro Selemam Mfinange, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Same Mashasriki, katika uzinduzi wa bonanza la vijana, lililoandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo Anne Kilango Malecela.
Mfinanga alisisitiza kuwa mikopo hiyo inalenga kuwasaidia vijana kuanzisha miradi ya kilimo na ufugaji ambayo itawawezesha kuwa na uchumi imara na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
"Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana ili kuwasaidia kujenga na kukuza uchumi wao kupitia sekta ya kilimo na ufugaji, hivyo ni jukumu lenu vijana kuchangamkia fursa hizi ambazo zimejitokeza," alisema Mfinanga.
Aidha, Mfinanga alieleza kuwa halmashauri ya Same inatoa mikopo hiyo bila riba; lengo ni kuwasaidia vijana kuwa na majukumu na kujenga ustawi wa jamii kupitia shughuli za uzalishaji.
Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango Malecela, alisema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya watu nchini ni kundi la vijana.
“Niko hapa kwa ajili ya kuwaeleza vijana wa Jimbo la Same Mashariki kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imeleta fedha nyingi sana za maendeleo ndani ya jimbo letu, ukiwemo mradi wa barabara ya Mkomazi-Kisiwani–Same inayojengwa kwa kiwango cha lami,”alisema.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Same Upendo Wella, aliwasihi vijana kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri katika kujiajiri na kuongeza kipato chao ili waweze kufikia maelego wanayoyatarajia.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 idadi ya Watanzania ilifikia zaidi ya milioni 60 ambapo Wanawake walikuwa milioni 31, sawa na asilimia 51 na Wanaume milioni 30, sawa na asilimia 49, huku idadi ya vijana takwimu zinaonesha kuwa kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 lilikuwa na idadi ya watu 21,312,411 sawa na asilimia 34.5 ya Watanzania wote.
Uzinduzi wa bonanza hilo ni sehemu ya juhudi za serikali na chama cha CCM kuhamasisha vijana wanashiriki katika shughuli za maendeleo, hasa katika sekta zinazoweza kuleta manufaa makubwa kwa taifa kama vile kilimo na ufugaji.









