KIBONG’OTO-SIHA
Serikali
imeelezea kuridhishwa na usimamizi mzuri wa utekelezaji miradi ya Kimkakati
iliyopo katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto
(KIDH), ambapo mbali na kuboresha huduma za afya pia thamani ya fedha zimeonekana
wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri
wa Afya Jenista Mhagama, aliyasema hayo Machi 1.2025, wakati alipotembelea hospitali hiyo iliyoko Wilaya
ya Siha mkoani hapa na kujionea mitambo mbalimbali ikiwemo mtambo wa kuzalisha
hewa tiba (Oksijen) uliogharimu kiasi cha Sh Bilioni 1.6.
Miradi
mingine aliyoitembelea ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la Ladiolojia
litakalotumika kwa ajili ya uchunguzi wa njia ya mawimbi sauti (MRI) lililogharimu
jumla ya Sh bilioni 8.5. na mradi wa kinu cha kuongeza uzalishaji wa umeme kwa
ajili ya matumizi ya hospitali hiyo unaogharimu kiasi cha Sh milioni 957.1.
Alisema
kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ya Kimkakati inaiwezesha Hospitali Maalum ya
Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto kupiga hatua kubwa kuelekea kuwa Taasisi
ya Magonjwa Ambukizi inayojitegemea.
Alisema
Tayari Tanzania imeshapiga hatua kubwa baada ya kufanya vyema kwenye kuboresha
afya ya msingi, utafiti na Ubingwa bobezi katika tiba na kwamba nia ya serikali
ni kuuonyesha ulimwengu kuwa Tanzania imejizatiti vyema katika eneo hilo la la
Magonjwa Ambukizi.
“Nipende kuwapa habari njema ya kuwa kukamilika kwa miradi hii umeiwezesha hospitali hii kupiga hatua kubwa kuelekea kuwa taasisi inayojitegemea”,.”alisema Waziri Mhagama.
Alisema
uwekezaji mkubwa uliowekwa hospitali ya Kibong’oto na Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais DK. Samia Suluhu Hassan, inaiwezesha KIDH kuwa na taasisi mahiri
itakayoshughulikia magonjwa ambukizi.
Pia Waziri
Mhagama alisema Serikali itapeleka mashine ya uchunguzi kwa njia ya mawimbi
sauti ambayo haitumii mionzi (MRI).
Akizungumzia mchango wa Serikali katika kuboresha huduma za afya hospitalini hapo Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk. Leonard Subi aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi ambazo alisema zimepelekea hospitali hiyo kupiga hatua kubwa katika kutoa huduma za afya.
Dk. Subi alisema serikali ilitoa Sh Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji wa hewa tiba ya oksijeni, ambapo mtambo huo unauwezo wa kuzalisha mitungi ya gesi 96 hadi 160 kwa siku.
“Tayari hospitali ya Kibong’oto imeanza kuzalisha hewa tiba ya oksijeni jambo ambalo limewezesha Taifa kuokoa Sh milioni 500 kwa mwaka ilizokuwa ikitumia kila mwaka kuagiza hewa tiba ya oksijeni”, alisema.
Aidha Dk. Subi alisema mbali na uzalishaji hewa tiba ya oksijeni, pia Serikali ilitoa Sh milioni 580 kwa ajili ya kusimika mtambo wa kichomea taka hospitalini hapo pamoja na mradi wa kinu cha kuongeza uzalishaji wa umeme kwa ajili ya matumizi ya hospitali.
“Kwa sasa uzalishaji umeme umeongezeka kutoka KV 100 hadi KV 1,000 jambo ambalo limechangia kuboresha huduma hospitali yetu ya Kibong’oto”.alisema Dk. Subi.
Aliongeza
kuwa katika kipindi cha miaka minne ya
uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan hospitali ya Kibong’oto imepata Sh bilioni 32
ambazo zimetumika kuboresha huduma za afya hospitalini hapo.
Aidha
DK. Subi aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kuridhia na kutoa
ushirikiano wake ambao unalenga kuifanya hosptali hiyo kuwa taasisi ya
kujitegemea ambapo alisema hiyo italifanya Taifa kupiga hatua kubwa katika
kuboresha sekta ya afya.
“Kwa sasa dunia nzima inapambana na magonjwa ambukizi hivyo kwa Tanzania kuwa na taasisi maalum ya magonjwa ambukizi na inayojitegemea ni hatua kubwa linapokuja kushughulikia magonjwa ambaukizi ya aina mbalimbali”, alisema.