Naibu Waziri Mkuu ; Awataka wadau wa Maendeleo kushirikiana na Waandaji wa Mbio za Kilimanjaro Marathon

USHIRIKA-MOSHI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko,  ametoa rai kwa wadau wa Maendeleo kushirikiana na Wandaajiwa Mbio za Kilimanjaro International Marathon ili kutumia mashindano hayo kuinua sekta ya utalii hapa nchini.

Dk. Biteko aliyasema hayo Februari 23,2025 mjini Moshi, wakati akihitimisha mbio hizo ambazo zimeingia msimu wa 23 tangua kuanzishwa kwake mwaka 2002.

Alisema taarifa zinaonesha kuwa ushiriki katika mashindano hayo unaongezeka kila mwaka; huku akitolea mfano mwaka 2024 ambapo jumla ya washiriki walioshiriki mbio hizo walikuwa 12, 800 na mwaka huu idadi hiyo imefikia zaidi ya 20,000.

Dk. Biteko aliwataka wananchi kuendelea kushiriki mazoezi mara kwa mara ili kuboresha afya zao na pia kuepuka maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa ni tishio ndani ya jamii katika miaka ya hivi karibuni.

Aidha aliwapongeza wadhamini wa mashindano hayo wakiwemo wafadhili wakuu Kilimanjaro Premium Lager na wadhamini wa mbio za kilomita 21 kampuni ya Yas Tanzania kwa kufanya mashindano hayo kuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi chote cha miaka zaidi ya 20.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi alisema mashindano ya Kilimanjaro Marathon yamepiga hatua kubwa katika kukuza michezo hapa nchini.

“Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na  waandaji wa Kilimanjaro International Marathon katika kutangaza utalii kutokana na Nchi ya Tanzania  kuwa na  vivutio vingi vya utalii.”alisema.

Aidha Waziri Kabudi alielekeza  Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kushirikiana na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuandaa mpango mkakati wa kuendelea vipaji vya mchezo wa riadha ili kuweza kupata vijana wengi zaidi watakao kuwa wakishiriki mbio hizo kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Waziri Kabudi alisema katika kutimiza azma hiyo Serikali inajenga viwanja vya kisasa vya mpira wa miguu Jijini Arusha na Dodoma ambapo vitakuwa na miundombinu ya mchezo wa riadha na kwamba viwanja hivyo vitakuwa na viwango vya FIFA na Olmpic ili kuwapa fursa wanariadha wa Kitanzania kujinoa kwa kufanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushindana Kimataifa.

Awali akizungumza Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania Silas Isangi,alisema  kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 mbio za nyika zimeendelea kufanya vizuri hapa nchini tofautia na kipindi cha nyuma.

Akitangaza matokeo ya washindi wa mbio hizo Kocha wa Timu ya Taifa ya Riadha Anthony Mwingereza,alisema Wanariadha wa Kitanzania wamenga’ra katika mbio za Kimataifa za Kilimanjaro mwaka huu, ambapo Hamis Misai alishinda nafasi ya kwanza mbio za kilomita 42.2 kwa muda wa saa 2:20:45.

Alisema  kwa nafasi ya pili ilichukuliwa na Aloyce Simbu wa Tanzania aliekimibia kwa muda wa saa 2:21:17, mbele ya Mkenya Abraham Kipkosgei wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 2:24:12.

Aidha alisema  kwa upande wa Wanawake nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Jacinta Chepkoech wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 2:45:39, akifuatiwa na Agnes Musabyimana kutoka Rwanda aliekimbia kwa muda wa saa 3:00:07 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Neema Sanka wa Tanzania aliekimbia kwa muda wa saa 3:00:49.

Alisema kwa upande wa mbio za kilomita 21.1 za Yas Kilimanjaro Marathon half-marathon, mshindi alikuwa ni Mtanzania Failuna Matanga aliekimbia kwa saa 1:17:37 na kumtangulia Irine Wawuda wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 1:18:44 mbele ya Mtanzania Neema Festo aliekimbia kwa muda wa saa 1:21:38.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.