Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imepiga hatua kubwa baada ya kuanzisha mradi wa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa kutumia panya buku.
Mradi huo ambao umeanzishwa kwa ushirikiano na na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) unalenga kuboresha mbinu za kugundua na kutibu Kifua Kikuu kwa njia ya kisasa na haraka zaidi.
Mkurugenzi wa KIDH Dk. Leonard Subi Aliyasema hayo jana, wakati wa kuutambulisha mradi huo ujulikanao kama SUA-APOPO ambao utaendeshwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Dk. Subi alisema Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto imepiga hatua kubwa katika shughuli za kitafiti ya magonjwa ambukizi mbali na zile zinazohusiana na Kifua Kikuu pekee.
Akizungumzia kuhusu mradi huo wa SUA-APOPO, Dk. Subi alisema kuwa Hospitali ya Kibong’oto, itautumia panya buku kwenye tafiti zake zinazolenga kugundua vimelea vya Kifua Kikuu kwenye makohozi.
Akiongelea mradi huo, Mratibu wa mradi wa SUA-APOPO Dk. Joseph Soka alisema mradi huo ulianzishwa mwaka 2002, ambapo alisema ulijumuisha Mataifa ya Tanzania, Msumbiji na Ethiopia wakati ukianza kutekelezwa.
Alisema kwa Tanzania mradi huo ulianzia mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, na Dodoma ukijumuisha jumla ya vituo 82 vilivyoko katika mikao hiyo.
Dk. Soka alisema mradi huo unahusika kugundua vimelea vya Kifua Kikuu kwa kutumia panya buku ambapo huchukua sampuli za makohozi ambayo yatakuwa yamepimwa kwenye vituo kwa kutumia teknolojia walizonazo kama vile GeneXpart na zile ambazo zitaonekana Negative wameleta teknolojia ya nyingine ya kuwatumia panya buku hao kwa ajili ya kugundua vimelea hivyo vya kifua kikuu.
Aidha alisema tangu kuanzishwa kwa mrdai huo, panyabuku wameshachunguza sampuli zaidi ya 1,000,000 ambapo kati ya hizo, sampuli 33,000 ziligundulika kuwa na vimlea vya kikua kikuu kupitia Panya buku.
“Mradi huu utakwenda kufanyika kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo mkoa wa Tanga, Manyara, Arusha na Kilimanjaro ambapo vituo zaidi ya 40 zitakwenda kutumika kwa ajili ya uchunguzi wa vimela hivyo kwa kutumia Panya buku ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro mradi huo utaanza rasmi Machi mwaka huu kwa vituo 10,”alisema Dk. Soka.
Akifungua semina hiyo iliyowahusisha waganga wakuu wa halmashauri za wilaya za mkoa, wataalam wa maabara, Waratibu wa Kifua kikuu na wauguzi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dk. Jahir Khanga aliupongeza uongozi wa Kibong’oto kwa kuanzisha mradi huo ambapo alisema utachangia kwa kiasi kikubwa ufanisi hospitalini hapo.
Dk. Khanga alisema mradi huo utakwenda kupungua gharama hizo haswa ikitiliwa maanani ya kuwa panya buku mmoja anaweza kupima sampuli 100 za vimelea kwa wahisiwa wa ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa muda wa dakika 10.
Awali akiutambulisha mradi huo Mratibu wa APOPO-SUA kutoka Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH),Dk. Peter Mbelele, ambapo alisema utumiaji wa panya hao utaweza kusaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wengi wa wahisiwa wa vimela vya Kifua Kikuu.
Dk. Mbelele alisema panya mmoja anauwezo wa kugundua kama sampuli ina vimelea vya kifua kikuu kwa muda wa sekunde moja, na hupima sampuli za makohozi 100 kwa dakika 20 na kwamba teknolojia hiyo inaweza kutumika hata kwenye upimaji wa sampuli nyingi kutoka kwenye kundi kubwa la watu (mass Screening) kwa muda mfupi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Kiliamnjaro Dk. Peter Nigwa, alisema Mradi huo utakwenda kuwanufaisha wananchi wengi kwa kuwaibua wahisiwa wengi wa ugonjwa wa kifua kikuu ambao huwa hawapatikani hasa kwa watoto ambao hawawezi kutoa makohozi yenye ubora unaohitajika.