DC Mnzava: Pazeni sauti kuzuia Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Wasichana

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Komredi Godfrey Mnzava akiwahutubia mamia ya wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi waliokusanyika mnamo tarehe 5 Machi 2025 katika viwanja vya KDC kuadhimisha Siku ya Wanawake inayofanyika kila mwaka tarehe 8 Machi. (Picha zote na Johnson Jabir/ KISENA Update)

MOSHI, KILIMANJARO

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava ameitaka Jamii kupaza sauti zao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyotendea wanawake na wasichana katika maeneo yao ili kudhibiti changamoto hiyo.

Akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Ulimwenguni ambayo hufanyika kila tarehe 8 Machi; kwa Halmshauri ya Wilaya ya Moshi yamefanyika Machi 5 katika viwanja vya michezo vya KDC amesema jamii inapaswa kutofumbia macho vitendo hivyo.

DC Mnzava amesema mpaka hatua ya mahakama kushughulikia kwa haraka na haki kwa watendewa kupatikana kwa wakati inaonyesha ni kwa namna gani serikali imedhamiria kwa dhati kutokomeza changamoto hiyo.

“Viongozi tumepewa dhamana tuhakikishe haki, usawa kwa wanawake; tuhakikishe vinatendeka wakati wote, yanapojitokeza matukio yoyote yale ya ubaguzi na yenye kuwaumiza wanawake pamoja na wasichana tusisite kuchukua hatua mara moja; tusinyamaze tutoe taarifa;” amesema DC Mnzava.

Akiwasilisha ripoti kuhusu Wanawake katika Halmshauri ya Moshi Afisa Maendeleo Stella Magori amesema jamii inapaswa kuendelea kutoa ulinzi kwa watoto wa kike kwani ndani ya kipindi kifupi matukio hayo yametokea.

“Ingawa juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia zinaendelea, lakini bado watoto wa kike wanatendewa vitendo vya ukatili ambapo Katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025  watoto wa kike 16 walifanyiwa ukatili wa kijinsia na matukio hayo yaliripotiwa katika vyombo vya kisheria ambapo matukio 13 yameshatolewa hukumu na mengine matatu yanaendelea mahakama,” amesema Bi. Magori

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya YA Moshi Morris Makoi amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kujitahidi kuwasaidia wanawake waliopo vijijini kupata mikopo ya asilimia tano isiyo na riba ikiwa ni mpango kamili uliowekwa kwa ajili ya kumwezesha mwanamke kiuchumi.

“Jitahidi kuwasaidia wamama kule vijijini kuhakikisha wanaweza kufikia malengo ya kuchukua mikopo ya asilimia tano bila riba; kwa kubadilisha uzoefu wakapata kwa wakati na hata kuirejesha,” amesema Makoi.

Awali DC Mnzava alishuhudia Bonanza la Michezo ikiwa kama kionjo katika kuadhimisha siku ya mwanamke, michezo kama kukimbiza kuku, kukimbia na magunia na kukimbia na yao katika kijiko kikiwa mdomoni ilikuwa ni burudani tosha kutoka kwa wanawake.

Pia mashindano ya unywaji wa soda katika bonanza hilo ambalo DC Mnzava aliwakabidhi washindi wa michezo hiyo vyeti vya kutambua mchango wao na Shilingi 10,000/= kila mmoja ambapo jumla ya washindi wapatao 15 walijipatia zawadi hizo kwenye bonanza hilo.

Kwa upande wao washiriki wa Siku hiyo iliyopambwa kwa Kauli mbiu, “Wanawake na Wasichana 2025, Haki, Usawa na Uwezeshaji,” wamesema ushiriki wa mwanamke katika kuijenga jamii ni mkubwa hivyo mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni vema yakaendelea ili kujenga jamii iliyo bora.

“Tunaishukuru Serikali yetu ya Mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mikopo isiyo na riba ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanawake pia kina mama wengi wameamka kuhusu ukatili wa kijinsia kutokana na elimu inayoendela kutolewa kwa jamii zetu,” amesema Reginald Ngowi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.