Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira na Maendeleo Kilimanjaro (KCDE) Dk. Padri Aidan Msafiri, akizungumza na Waandishi wa Habari ofsini kwake, kuhusiana na kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti.
MOSHI-KILIMANJARO
Jamii imeshauriwa kutumia maadhimisho ya matukio muhimu kupanda miti ili kuboresha mazingira, jambo ambalo litachangia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yamesemwa Machi 15,2025 na Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Mazingira na Maendeleo Kilimanjaro (KCDE) Dk. Padri Aidan Msafiri, wakati akizungumzia shughuli za upandaji miti utakaofanyika kama maadhisho ya miaka 62 ya kuzaliwa kwake.
Dk. Msafiri alisema kuwa, ili kuhakikisha mazingira na uoto wa asili unalindwa kwa manufaa endelevu ya Mwanadamu na viumbe hai, jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na uoto wa asili kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kwa viumbe hai.
“Kuna matukio mengi ya kitaasisi na hata kifamilia hapa nchini kwetu ambayo kama yakiadhimishwa kwa kupanda miti, Mkoa wa Kilimanjaro utakuwa na mazingira mazuri yatakayowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi”, alisema Dk. Msafiri.
Alisema kwa upande wake, katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa amepanga kushirikiana na wenzake katika kupanda miti kama sehemu ya maadhimisho hayo kupitia Kauli Mbiu ya Kukijanisha Kilimanjaro.
“Kuelekea siku ya kumbukumbu ya miaka 62 ya kuzaliwa kwangu Machi 28, mwaka huu, taasisi ya KCDE, itapanda miti aina mbalimbali maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro ikiwemo ya matunda kwa lengo la kuboresha mazingira chini ya Kauli Mbiu, ‘Otesha na tunza miti rafiki wa mazingira Punguza Joto Kilimanjaro”, alisema na kuongeza, kauli mbiu hiyo inalenga kuboresha maisha kupitia upandaji wa miti.
Aidha alitoa rai kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona jinsi ya kuifanyia marekebisho sheria ya mazingira ili kuwe na sheria ambazo zitakabiliana na uharibifu wa mazingira.
“Uharibifu wa mazingira unaenda kasi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma ni vyema watunga sheria kuona umuhimu wa kushirikiana na wadau wa mazingira na wale wa sheria ili kuja na sheria ambayo itasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira nchini”, alisema.
Dk. Msafiri pia alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya kisiasa hapa nchini kutumia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu kwa kutangaza sera ambazo kipaumbele chake kitaboresha mazingira hapa nchini.
“Viongozi hao wa kisiasa pia watumie muda wa kampeni za uchaguzi mwaka huu, kupanda miti kabla ya kupanda majukwaani kunadi sera zao”, alisema na kuongeza, zoezi hilo lifanyika kabla ya mikutano yote ya kampeni ya ngazi zote zinazowaniwa.

