MOSHI-KILIMANJARO.
Ligi ya soka ya mpira wa miguu kwa wanawake mkoa wa Kilimanjaro msimu wa 2025/2026 inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kwa michezo sita katika viwanja tofauti.
Katibu wa soka la Wanawake mkoa wa Kilimanjaro Salma Omari Mndaira, ameyasema hayo Machi 14, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea ufunguzi wa ligi hiyo itakayofanyika Machi 15 mwaka huu.
Amesema katika mechi ya ufunguzi timu ya Masumbeni kutoka Wilaya Mwanga, itaikaribisha timu ya Kurugenzi kutoka wilaya ya Same kwa ajili ya ufunguzi wa ligi hiyo ambayo itakayofanyika siku ya Jumamosi ya Machi 15 mwaka huu uwanja wa CD-Msuya, majira ya saa kumi jioni.
Mndaira amesema timu ya Rombo Queen itaanza ugenini dhidi ya Kili Wonders Machi 16 mwaka huu kwenye uwanja wa Rombo.
Amesema timu ya MUCO Queen inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kili Plantation Machi 29 kwenye Uwanja wa Moshi huku Kurugenzi ikiikaribisha Masumbeni kwenye Uwanja wa Same Machi 22 mwaka huu.
Aidha amesema Kili Wonders watakuwa wenyeji wa Rombo Queen Machi 23 ambapo mtanage huo utapigwa uwanja wa Moshi.
Miamba mingine ya soka la wanawake ni Kili Plantation dhidi ya MUCO Queens itakayomenyana Machi 30 katika uwanja wa Gomberi.
Akizungumzia umuhimu wa ligi hiyo Katibu huyo amesema kuwa ligi ya soka ya mpira wa miguu kwa wanawake inamwezesha mtoto wa kike kuweza kutoka nje ya mkoa na kwenda kuipeperusha bendera ya mkoa wa Kilimanjaro kupitia soko la wanawake.



