KIBONG’OTO-SIHA
Taasisi isiyo kuwa ya
Kiserikali ya SUA-APOPO, imesaini makubaliano (MoU) na Hospitali Maalum ya
Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maabara ya
panya, itakayohudumia wahisiwa wa vimelea vya Kifua Kikuu katika mikoa ya Kaskazini.
Mratibu wa SUA-APOPO,
Dk Joseph Soka, aliyasema hayo jana wakati wa kusaini makubaliano hayo na
kusema kuwa mradi huo unalenga kuboresha mbinu za kugundua na kutibu kifua
kikuu kwa njia ya kisasa na haraka zaidi.
Dk. Soka alisema kuwa
maabara hiyo itagharimu takribani Sh Bilioni 1, ambapo pia itahusisha ajira ya
watumishi 12, kutoa mafunzo kwa waratibu wa kifua kikuu pamoja na watumishi wa
afya ili kuboresha ufanisi wa kugundua kifua kikuu kwa usahihi.
“Leo SUA-APOPO
tumeingia makubaliano na KIDH, ili kuanza ujenzi wa maabara ya panya buku,
ambayo itagharimu jumla ya Sh takribani bilioni 1, maabara hii itakuwa
ikihudumia wahisiwa wa kifua kikuu kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na
Kilimanjarao.”alisema Dk. Soka.
Alisema mradi huo pia
utahusisha vituo 40 vya mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kwa
mkoa wa Kilimanjaro utakuwa na vituo 10 kutoka katika hospitali za wilaya ya
Siha, Moshi vijijini, Manispaa ya Moshi, Same, Hai pamoja na vituo vyas afya.
Alisema “Vituo hivi
vitakuwa vinakusanya sampuli za makohozi na kuvisafirisha kwenda Hospitali
Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto kwa ajili ya kuchunguzwa na
Panya Buku pamoja na vipimo vilivyothibitishwa nchini kama vile Hudubini,
GeneXpert na kuotesha kwenye vitalu vya kifua kikuu (MGITn L J).
Alisema panya buku hao
wana uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya kifua kikuu hata kwa mtu ambaye
alifanya vipimo hospitalini kama vile vya Hadubini (Smear
Microscopy) na mashine za kupima vina saba mfano wa GeneXpert na vipimo
vingine na kunatoa majibu kuwa hana kifua kikuu lakini panya buku hao wana
uwezo wa kubaini vimelea ambavyo mashine za hospitalini zinaweza
zisibaini.
Alisema, utumiaji wa
panya hao, unaweza kusaisdia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wengi zaidi kwani
panya mmoja ana uwezo wa kugundua kama sampuli ina vimelea vya kifua kikuu kwa
muda wa sekunde moja na hupima sampuli za makohozi 100 kwa muda wa dakika 20.
Alisema teknolojia
mpya hiyo hiyo inaweza kutumika hata kwenye upimaji wa sampuli nyingi kutoka
kwenye kundi kubwa la watu.
Akizungumzia mafunzo
ya panya buku hao, Dk. Soka alisema mafunzo yao huchukua muda wa miezi 9
hadi mwaka mmoja tangu akiwa na umri wa mwezi mmoja na
anaweza kufanya kazi kuanzia akiwa na umri wa mika miwili hadi miaka 10.
“Panya buku mmoja
anaweza kupima sampuli 100 kwa dakika 10 hadi 20, panya buku huwa anagundua TB
kwa kunusa compound “Volatile organic compound (VOC) ambayo ipo kwenye
kimelea au bacteria anayesababisha kifua kikuu yaani (Mycobacterium
tuberculosis) kwa kunusa VOC hiyo, lakini pia panya buku huyo anauwezo wa
kutofautisha vimelea vya kifua kikuu na vimelea vingine.
Dk. Soka alisema panya
buku; hawezi kuambukizwa TB kwa kuwa kabla hajanusa makohozi huwa
yanachemshwa (Autoclaved) kwenye jotoridi lenye nyuzi 100 kwa
dakika 40 joto ambalo lina weza kuuwa vimelea.
Awali akizungumza
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kiambukiza Kibong’oto (KIDH),Dk. Peter
Mbelele alisema utumiaji wa panya hao unaweza kusaidia kuongeza ugunduzi wa
wagonjwa wengi wa wahisiwa wa vimela vya Kifua Kikuu katika mikoa ya Kanda ya
Kaskazini.
Naye Mratibu wa Kifua
Kikuu na Ukoma Mkoa wa Kiliamnjaro Dk. Peter Nigwa, alisema Mradi huo utakwenda
kuwaibua wahisiwa wengi wa ugonjwa wa kifua kikuu ambao huwa hawapatikani
hususani watoto wadogo, ambao hawawezi kutoa makohozi yenye ubora unaohitajika.
Akizungumza Mtafiti
upande wa Vipimiolojia kutoka Shirika la Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu kituo
cha Mwanza (NIMR) Profesa Said Kapiga, alisema utumiaji wa teknolojia mpya ya
panya buku itakwenda kusaidia namna ya kuwagundua watu ambao wameambukizwa na
vimelea vya kifua kikuu.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH)
Dk. Leonard Subi, alisema hitaji la KIDH ni kuona ushirikiano katika mapambano
dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, hususan kwenye kifua kikuu wanayaendeleza.
Mradi huo wa kutumia
wanyama aina ya panya buku unatarajiwa kuongeza ufanisi mkubwa katika tafiti
mbalimbali za maradhi yanayoikabidi jamii.


