
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Dk. Joseph Kizito Mhagama, akizungumza Machi 15,2025 Wilayani Romba badada Wajumbe wa Kamati hiyo kutembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Rombo.
ROMBO-KILIMANJARO.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria, imeelezea kurishwa kwake na
usimamizi mzuri wa fedha zilizoidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini
(TAKUKURU).
Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Dk. Joseph Mhagama aliyasema hayo Machi 15,2025 wakati Wajumbe wa Kamati hiyo
walipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi ya TAKUKURU Wilayani Rombo,
Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema uamuzi huo
unalenga kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo, ambayo ni muhimu katika
kupambana na rushwa na kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali za umma, hatua ambayo
inadhihirisha dhamira ya Rais Samia Suluhu katika kuimarisha taasisi za umma na
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Kamati hiyo imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa kuridhia kutoa eneo ambalo limetumika kwa ajili ya huduma kwa Watanzania kupitia TAKUKURU, huku akisistiza kuwa hatua hiyo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya serikali za mitaa na taasisi za umma.
Akiwasilisha taarifa ya kwa Kamati hiyo, Naibu Waziri, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ma Utawala Bora Deus Sangu, alisema kuwa jumla ya Sh milioni 299.9 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Rombo, Mkoani hapa.
“Makadirio ya gharama ya mradi yalikuwa ni Sh milioni 299.9; hadi kukamilika kwake mradi ulitumia kiasi cha Sh milioni 290.1 na kubaki Sh milioni 9.8, sawa na asilimia 3.26 ya makadirio ya gharama ya utekelezaji wa mradi huo.”alisema Naibu Waziri Sangu.
Alisema kutokana na
kuwepo kwa bakaa ya fedha, waliamuliwa kuongeza kazi ya kusawazisha ardhi
(landscaping), kuweka “paving blocks” na kuweka kinga ya pembeni katika njia ya
watu wenye ulemavu (balustrades).
Aliongeza kuwa fedha za ujenzi huo ni sehemu ya Sh bilioni 4.5 ambazo ziliidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya ya TAKUKURU na ukarabati wa yale ya zamani hapa nchini.
Aidha Naibu Waziri Sangu, alisema kuwa ujenzi wa jengo la Rombo ulianza kutekelezwa Januari, 2024, kwa utaratibu wa Force Account chini ya ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Rombo kwa pamoja na kitengo cha usimamizi wa Milki cha Makao Makuu ya TAKUKURU.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Francis Chalamila alilipongeza Bunge kwa kuidhinisha fedha ambazo zinaiwezesha TAKUKURU kuwa na majengo yake kama taasisi.
Chalamila alisema kwa kutambua ukubwa wa changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana nayo ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya.
Alisema hadi kufikia Februari, 2025, TAKUKURU ilikuwa inamiliki jumla ya majengo 68, ambapo kati ya hayo, Majengo 21 ni kwa ajili ya ofisi za Mikoa, 46 ni ofisi za wilaya na jengo moja ni la kituo maalum, huku akisema kuwa taasisi hiyo imepanga katika majengo 60 kwa ajili ya ofisi za Mikoa, wilaya na vituo maalum.
Aidha alisema kuwa katika mwaka fedha wa 2024/25 Bunge limeidhinisha jumla ya Sh Bilioni 6 kwa ajili ya kutekeleza miradi 21 ya ofisi za TAKUKURU hapa nchini.












