Watoa huduma ngazi ya jamii mkoa wa Kilimanjaro wapongezwa

MOSHI-KILIMANJARO.

Watoa huduma ngazi ya jamii mkoa wa Kilimanjaro, wamepongezwa kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuelimisha wananchi kuhusu masuala mazima ya afya, jambo ambalo limezidi kutoa chachu kwa wanajamii kuhudhuria katika vituo vya afya.

Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma mkoa wa Kilimanjaro Dk. Peter Nigwa, alitoa pongezi hizo Machi 17,2025 wakati akizungumza katika mahojiano maalumu, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 24 ya kila mwaka. 

Alisema watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa wakisaidia sana katika kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu ambapo takwimu za mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka 2024 zinaonesha kwamba mkoa uliweza  kugundua wagonjwa wa Kifua Kikuu takribani 3,600 ambao waliweza kuanzishiwa matibabu.

Aidha  alisema mkoa unaendelea kutekeleza afua mbalimbali kulingana na mpango wa Kitaifa wa kuharakisha uibuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa kuwabaini mapema wateja ambao ni wahisiwa wa kifua kikuu.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani iliyobeba Kauli Mbiu “Kwa Pamoja Tunaweza Kutokomeza Kifua Kikuu, Azimia Wekeza na Timiza.” Dk. Nigwa alisema kuwa mkoa huo, unaendelea na utoaji wa elimu ya kifua kikuu kwenye shule zote za msingi na sekondari zilizoko katika wilaya zote za mkoa huo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa mwaka 2023 takribani watu milioni 10.8 walipata maambukzi ya Kifua Kikuu na kati yao watu milioni 1.25 waliweza kupoteza Maisha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.