Serikali imetoa kiasi cha Sh Bilioni 16.8 kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji eneo la Kigonigoni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Hayo yameelezwa Machi 20,2025 na Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani humo, Joseph Tadayo wakati akizungumzia maswala ya maendeleo jimboni humo.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa fedha, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mkoa wa Kilimanjaro, kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi wa Skimu ya umwagiliaji Kigonigoni wenye Thamani ya Tsh 16. 874.
Tadayo aliutaja mradi huo kuwa wa pili kwa ukubwa kati ya miradi iliyoko wilayani humo, ukitanguliwa na Mradi wa Mwanga-Same-Korogwe.
Alisema mradi unaoshika nafasi ya Tatu ni wa Barabara ya Msuya bypass wa Sh Bilioni 13, kisha Stendi ya mabasi na mradi wa Hospitali mpya ya wilaya.
Alizungumzia manufaa ya mradi huo, Mbunge Tadayo alisema kuwa mbali na kuwa chanzo cha kuongezeka kwa mazao ya chakula, pia skimu hiyo itakuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wananchi.
Alisema tayari amefanya mazungumzo na uongozi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), kuhusu kutumia skimu hiyo kuzalisha miwa kwa ajili ya kilimo biashara jambo ambalo bodi hiyo wamelikubali.
Alisema kuwa kilimo hicho kitakuwa ni kwa njia ya mkataba ambapo wakulima watalima miwa na kisha bodi ya sukari itawaunganisha na viwanda vya uzalishaji wa sukari jambo ambalo litawaongezea kipato.
Alisema kuweko na skimu hiyo ya umwagiliaji Kigonigoni kutawezesha kuwa na fursa nyingi za kilimo cha umwagiliaji jambo ambalo litawaongezea wananchi wa wilaya ya Mwanga mapato pamoja na serikali kupitia kodi mbalimbali zitakazotokana na mauzo ya mazao yatakayozalishwa kupitia skimu hiyo.
Alisema mbali na skimu hiyo pia serikali imeleta jumla ya Sh Bilioni 1.8 kwa ajili ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji Kambi ya Swala ulioko kata ya Kirya na Sh Bilioni 4 zingine kwa ajili ya mradi mwingine wa umwagiliaji katika kata ya Kileo.
Aidha Mbunge huyo alitoa wito kwa wananchi wilayani humo hususan vijana kushirikiana wakati wa utekelezaji wa mradi huo kutokana na ukweli kuwa utakuwa na manufaa ya kiuchumi kwao na wilaya kwa ujumla.



