MWANGA-KILIMANJARO.
Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea hospitali mpya ya wilaya ukanda wa tambarare yenye miundombinu na vifaa vya kisasa.
Akizungumza mmoja wa wakazi wa mji mdogo wa Mwanga Hemed Suleiman, alisema wananchi wa ukanda wa tambarare wakiugua walikuwa wakipelekwa ukanda wa milimani maeneo ya Usangi ilikokuwa imejengwa hospitali ya wilaya.
Alisema kujenga hospitali mpya ya wilaya, ukanda wa tambarare, imerahisisha upatikanaji wa matibabu na kupunguza safari za kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya matibabu.
Awali akizungumza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Dk. Serijo Kusekwa, alisema Halmashuri hiyo ilipokea Sh bilioni 3.1 kati ya fedha hizo Sh milioni 153.5 kutoka mapato ya ndani.
Akizungumzia ujenzi wa awamu ya tatu ya Majengo ya hospitali hiyo Dk. Kusekwa alisema mradi huo unahusisha umaliziaji wa majengo matano likiwemo jengo la kufulia, jengo la kichomea taka, kuhifadhia miili, na jengo la wodi ya baba, mama na mtoto.
“Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga inatoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mwanahamisi Munkunda alisema Wilaya hiyo imepokea Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo yaliyokuwa yamebaki kwenye utekelezaji wa mradi huo.

