TOROHA-MWANGA.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta ya
utalii kwa nia ya kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika sekta hiyo.
Waziri Mkuu aliyasema hayo Machi
25,2025 wakati wa hafla ya kuzindua lango la Ndea lililopo Kata ya Toroha kwa upande
wa Wilaya ya Mwanga katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi (MKONAPA).
“Serikali ya awamu ya sita
chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha sekta ya
utalii kwa nia ya kuboresha uchumi wa Taifa na kuongeza ajira”, alibainisha.
Aliongeza, "Katika
kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, serikali imetangaza utalii
kama sekta muhimu kwa kuzingatia mikakati ya uchumi wa nchi".
Aliendelea kusema kuwa
ushiriki wa Rais Samia, katika kuboresha sekta hiyo kupitia filamu ya Tanzania
Royal Tour ulikuwa muhimu na kwamba uamuzi wake umewahamasisha Watanzania
wengine kufanya kazi kwa bidii katika kuboresha sekta ya utalii.
"Serikali itaendelea kuifanya sekta ya utalii kuwa sekta kuu kwa kutangaza vivutio vya utalii vya nchi nje ya nchi ili kuifanya sekta hiyo kuendelea kuiingizia nchi mapato", aliongeza.
Akizungumzia lango la NDEA lililozinduliwa, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa ni nafasi nzuri ya kufungua fursa za kiuchumi katika wilaya ya Mwanga.
“Nichukue fursa hii kuwashauri
wakazi wa Wilaya ya Mwanga kuchangamkia fursa za biashara zitakazotokana na
kufunguliwa kwa Lango la Ndea kutokana na ukweli kwamba idadi ya watalii
wanaoingia Mkomazi kupitia Mwanga itaongezeka,” alisema.
Waziri Mkuu pia aliupongeza
uongozi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa maboresho makubwa iliyoyafanya na
kuchangia ongezeko la watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
“Tumeshuhudia katika miaka ya
hivi karibuni TANAPA ikileta maboresho na ubunifu mbalimbali ambao kwa namna
moja au nyingine umechangia kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi
hivyo kuchangia ongezeko la ajira na mapato ya Serikali kupitia sekta ya
utalii,” alisema.
Aliongeza, “Nichukue fursa hii kuwashauri (TANAPA) kuwaelimisha wakazi wa Mwanga aina ya biashara zitakazowafaa wateja wa kitalii ili waweze kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na wingi wa watalii watakaokuwa wakitumia lango la Ndea ili waweze kuboresha maisha yao kupitia biashara watakazofanya katika eneo hili.
Katika taarifa yake kwa Waziri Mkuu kuhusu mradi wa lango la Ndea, Mhifadhi Mkuu wa MKONAPA Emmanuel Moirana, alisema kuwa mradi huo wa lango uligharimu jumla ya shilingi milioni 350 na kwamba moja ya faida zake ni ongezeko la watalii wanaotembelea MKONAPA ambao alisema sasa watatumia lango hilo.
“Idadi ya watalii wa MKONAPA
imeongezeka kutoka zaidi ya watalii 3,300 mwaka 2020 hadi zaidi ya watalii
9,600 mwaka jana; tuna matumaini kuwa idadi ya watalii itaongezeka kutokana na
kuanzishwa kwa lango la Ndea kutokana na ukweli kwamba watalii kutoka Arusha na
wilaya za Moshi watakuwa na urahisi wa kuingia MKONAPA tofauti na siku za
nyuma”, alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mwanga
Wakili Joseph Tadayo, amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kuchangamkia fursa za
kiuchumi zinazotokana na watalii watakao kuwa wakipitia lango la Ndea wakiende
kutembelea hifadhi ya Mkomazi.
“Wananchi wa kijiji cha Karambandea Kata ya Toroha
Wilaya ya Mwanga, wanapaswa kujiandaa na kuchangamkia fursa hii ya utalii
kupitia lango la Ndea kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa sababu italeta mabadiliko
makubwa ya kiuchumi, wakinamama waone nafasi ya kupika vyakula vya asili,
kusuka mikake na kufinyanga vyungu,”alisema Mbunge Tadayo.
Aidha alisema kutoka lilipo lango la Ndea kwenda kwenye mradi wa kuzalisha Faru Weusi ni kilometa nane tu tofauti na kutumia malango mengine na kwamba uwepo wa lango hilo na kuishukuru serikali kwa kukubali kulifungua lango hilo.




