MAJALIWA; APONGEZA UWEKEZAJI ULIOFANYWA NA PROF. NGOMA

KWAKOA-MWANGA.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi binafsi katika kutoa huduma za afya ili huduma hizo ziweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo Jumanne, wakati akizindua kituo cha afya cha Mama Ngoma kilichoko kata ya Kwakoa, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu,; alikuwa akijibu ombi la Mkurugenzi wa taasisi hiyo Profesa Twalib Ngoma linalohusu kituo hicho kupewa fursa ya kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za afya.

“Sera ya afya inatoa nafasi kwa serikali kushirikiana na taasisi zingine zisizo za kiserikali lakini mara nyingi imeonekana kutumika kwa ushirikiano na taasisi za kidini tu; sera hii pia inatoa nafasi kwa watu binafsi kufanya ushirikiano huo”, alisema Waziri Mkuu.

Alisema “Ushirikiano na Serikalini katika kutoa huduma za afya sio jambo geni; Wizara ya Afya itumie Kanuni zinazotumika wakati wa ushirikiano na taasisi zingine zikiwemo zile za Kidini ili zitumike na kituo cha Mama Ngoma”, alisema.

Aidha Waziri Mkuu, aliiagiza Wizara ya Afya kuharakisha mchakato utakaoipandisha hadhi kituo cha Mama Ngoma kuwa hospitali kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa.

“Natoa agizo kwa Waziri wa Afya, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali na Msajili wa hospitali wakutane na mimi ofisini haraka iwezekanavyo ili wanieleze ni lini kituo cha Mama Ngoma kitapandishwa hadhi na kuwa hospitali”, alisema na kuongeza uwekezaji wa bilioni tano ni mkubwa sana kwa sekta ya afya.

Alisema kuwa, kupandishwa kwa hadhi ya kituo hicho cha afya kitawasaidia Wananchi wa Wilaya ya Mwanga na wale wanaotoka nje ya Mwanga pia kupata huduma za afya karibu zaidi na kumpa msukumo mwekezaji kwa maeneo machache kuendelea kuyaboresha.

Aidha Waziri Mkuu, alimpongeza Mkurugenzi wa kituo hicho cha afya Profesa Twalib Ngoma kwa kuamua kujenga kituo hicho cha afya ambacho kinatoa huduma muhimu ya afya kwa wananchi.

Kwa upande wake Profesa Ngoma alisema kuwa hospitali hiyo ilianzishwa ikiwa ni kuitikia wito alitoa hayati mke wake uliomtaka aanzishe kituo cha kutoa huduma za afya.

“Ujenzi wa hospitali hii ulianza mwaka wa 2011 na umegharimu Shilingi Bilioni 5 na tayari umeshaanza kutoa huduma kwa ajili ya wagonjwa wa nje, hospitali ina maabara, ina sehemu ya upasuaji pamoja na zile za huduma ya Mama na Mtoto”, alisema na kuongeza, huduma hizi tunatoa kwa ushirikiano mkubwa na halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.

Prof. Ngoma aliendelea kusema kuwa tangu kukamilika kwake tayari kimeshatoa huduma kwa mama wajawazito 45, wagonjwa wa nje 1,640 na wagonjwa wa kulazwa 330.

Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo alimshukuru Profesa Ngoma kwa kufanya uwekezaji huo ambao alisema unaunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuboresha afya za wananchi hapa nchini.

“Moja wapo ya sifa nzuri za serikali ni kutoa fursa kwa wananchi wake kuwekeza; fursa hii imempa nafasi Pro.f Ngoma kufanya uwekezaji huu ambao utasaidia kuokoa maisha ya watu wengi” alisema Wakili Tadayo.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.