UONGOZI wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) umepongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kuwa moja ya vipaumbele vya serikali yake.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 28,2025 na Mkurugenzi wa Bodi hiyo Mhandisi Segule Segule, wakati wa kikao cha mapendekezo ya majina ya Wajumbe wa Bodi ya 11 ya Maji Bonde la Pangani, mkutano uliofanyika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
“Rais Samia amefanya uhifadhi wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji kuwa moja wapo ya agenda muhimu ya serikali ya awamu ya sita na zaidi ya hayo yeye mwenyewe yuko mstari wa mbele kufuatilia maswala yote yanayohusiana na maswala haya mawili kila mara”, alisema.
Mhandisi Segule aliendelea kusema “Rais Samia amejikita moja kwa moja kwenye maswala haya sasa ni ajenda ya kitaifa na hili linawapa wepesi wale wote walio katika harakati za kutunza mazingira kutokana na ukweli kuwa kiongozi mkuu wa nchi ni kinara katika harakati za maboresho, utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji”.
Mhandisi Segule aliendelea kusema kuwa PBWB itaendelea kuhifadhi vyanzo vya maji kupitia njia mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti na pia kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Nzowa, Mhandisi Jackson Masaka kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro alitoa rai kwa wale watakaochaguliwa kuiongoza Bodi ya PBWB kuzingatia weledi na uadilifu wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Maji na matumizi yake ni muhimu sana kwa wananchi na Bodi ya Maji Bonde la Pangani imepewa jukumu la kusimamia raslimali hii muhimu, hivyo na nyinyi mtakaopewa jukumu la kuisimamia raslimali hii ni vyema mkahakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia uadilifu wa hali ya juu”, alisema.
Aidha Mhandisi Masaka aliwaasa Wajumbe hao watapakapokabidhiwa wajibu wa kuiongoza bodi hiyo, wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Raslimali za Maji namba 11 ya mwaka wa 2009.
Katika kikao hicho Mhandisi Masaka aliupongeza uongozi wa PBWB kwa kufanya shughuli zake kwa kutumia dhana ya ushirikishi jambo ambalo alisema linachangia kuweko kwa amani miongoni mwa watumia maji.
“Kwa mfano kwa kushirikiana na wenzenu walioko kwenye sekta ya ardhi wakati wa kutekeleza majukumu yenu kunawawezesha watendaji wa ofisi ya ardhi kutoa vibali maeneo yaliyo sahihi na ambayo hayaingiliani na meneo yenye vyanzo vya maji jambo ambalo linaepusha migogoro kati ya PBWB na wananchi”, alisema.
Katika kikao hicho Wajumbe wa kikao hicho walipendekeza majina ya watu 16 ambapo kati ya hayo, Waziri mwenye dhamana ya Maji atateua miongoni mwao kuunda Bodi ya 11 ya PBWB na ambayo inatarajiwa kuingia kazini Aprili, mwaka huu.