MOSHI.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Kilimanjaro, umetoa wito kwa waamini wake kutumia baraka walizopata kupitia mfungo wa Ramadhan kuliombea Taifa liendelee kuwa na Amani.
Sheikh wa mkoa wa Kilimanjaro Shaabani Mlewa, aliyasema hayo MAchi 27,2025 wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ambapo aliwaasa waamini kuliombea Taifa ili uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, uwe wa utulivu na Amani.
Akizungumza kwa niaba ya Sheikh wa Mkoa, Katibu wa Bakwata Mkoa wa Kilimanjaro Alhaj Awadh Lema, alisema “Amani yetu ni muhimu kuliko mtu mmoja mmoja na ndiyo inatufanya kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa letu vizuri; sisi viongozi wa dini hatutaruhusu Amani ivurugike”, alisema Alhaji Lema.
Katika hatua nyingine Alhaj Awadhi Lema, alimshukuru Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu kwa kuwaalika viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kushiriki Futari hiyo.
“Nashukuru hapa tumealikwa viongozi wa Kidini wa madhehebu mbalimbali, nitoe rai kwenu tushirikiane na serikali katika kuhakikisha amani tuliyonayo inaendelea kutamalaki; tusingojee amani itoweke ndiyo viongozi waanze kututafuta ili kuangallia jinsi ya kurudisha Amani iliyopotea”. Alisisitiza Alhaji Lema.
Alhaj Lema aliendelea kusema kuwa uongozi wa Bakwata utaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kupitia mahubiri kuhusu umuhimu wa kuitunza amani iliyoko hapa nchini popote pale wanapokutana na mtu zaidi ya mmoja ili elimu hiyo ienee kote kwa manufaa ya wananchi wote.
Akiongea katika hafla hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na teknolojia Profesa Adolf Mkenda, alimpongeza Mkuu wa Mkoa Nurdin Babu na familia yake kwa kuandaa futari hiyo ambayo alisema imejumuisha watu wa kada mbalimbali ikiwemo wa vyama vingine vya kisiasa.
“Hafla hii uliyoandaa pamoja na washiriki wake kutoka kada na tabaka mbalimbali ndani ya jamii, imeonyesha kwa vitendo Imani iliyojengeka miongoni mwa Watanzania ya kuheshimiana na kushirikiana kila mara inapotokea fursa ya kukutana”, alisema Prof. Mkenda.
Aidha Prof. Mkenda alisema hafla hiyo imeonyesha kwa vitendo dhana ya kuheshimiana na ushirikiano miongoni mwa dini na madhehebu mbalimbali jambo ambalo alisema limeonyesha kuwa msingi wa umoja uliowekwa na waasisi wa Taifa la Tanzania unaendelea kuweko.
Kwa upande wake Mwenyeji wa hafla hiyo RC Babu aliwashukuru wote waliohudhuria hafla hiyo, jambo ambalo alisema linaashirikia ushirikiano ulioko miongoni wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro.“Nichukue fursa hii pia kutoa pongezi kwa wenzangu ambao tunafanya nao kazi pamoja katika sekratrieti ya Mkoa kwa ushirikiano wao, ambao unatupa fursa ya kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro maendeleo”, alisema.
Babu aliwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ya kuwa uongozi wa Mkoa huo umejipanga vyema wakati wa kuelekea Sikukuu zinazotarajiwa kuadhimishwa hivi karibuni.